FBI yamkamata mshukiwa wa vifurushi 12 vyenye vilipuzi

Jeff Sessions. Pembeni ni picha ya mshukiwa Cesar Sayoc

Mwanasheria Mkuu wa Marekani Jeff Sessions amesema maafisa wa upelelezi wa serikali ya Marekani (FBI) wamemkamata mtu mmoja anayeitwa Cesar Sayoc, 56, anayeishi mji wa Aventura, Jimbo la Florida,arekani FBI, anayeshukiwa kuhusika katika tukio la kutuma vifurushi 12 vilivyo na vifaa vyenye uwezo wa kulipuka.

Kadhalika vifurushi vingine viwili vilivyo kuwa vimetumwa kwa seneta wa chama cha Demokrat Cory Booker na aliyekuwa mkurugenzi wa idhara ya ujasusi ya kitaifa James Clapper, vilikamatwa.

Maafisa wa FBI wanasema kwamba vifurushi hivyo vinavyo fanana na mabomu yaliyo tumwa kwa maafisa wengine wa ngazi ya juu, nchini Marekani, vilikamatwa katika jimbo la Florida kabla ya kuwafikia walengwa.

Wengine waliolengwa katika tukio la kutumwa mabomu ni Rais mstaafu wa Marekani Barack Obama, na waziri wa mambo ya nje wa zamani Hillary Clinton, maafisa wengine wa chama cha Democrat, wakosoaji wa Rais Donald Trump na shirika la habari la CNN.

Maafisa wamefanikiwa kukamata mabomu hayo kabla ya kuwafikia walengwa.

Rais Donald Trump amelaumu vyombo vya habari kwa kuongezeka kwa hali ya chuki za kisiasa nchini Marekani, ambayo wachambuzi wanasema imeleta uhasama na majaribio ya kuuwa.