Ethiopia : Waziri Mkuu adaiwa kukabiliwa na mtihani wa uchaguzi

Wananchi wa Ethiopia wakipiga kura katika kituo cha kupiga kura mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, Jumatatu, Juni 21, 2021.

Ethiopia imepiga kura Jumatatu katika kile kinachoonekana kuwa mtihani mkubwa wa uchaguzi kwa Waziri Mkuu wa sasa Abiy Ahmed.

Foleni ndefu za wapiga kura zilionekana katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu, Addis Ababa, wakati hali ya usalama ikiwa imeimarishwa kote nchini.

Zaidi ya Waethiopia milioni 37 walitarajiwa kupiga kura. Eye-rusalem Meshesha, ni mkazi wa Addis Ababa, na ni kati ya wale walioshiriki katika uchaguzi huo.

Meshesha anasema : "Hii ni siku ya maamuzi kwa Ethiopia. Natumai kila kitu kitakuwa sawa, na amani itashinda baada ya uchaguzi huu. Baada ya uchaguzi huu, kutakuwa na serikali mpya. Kwa hivyo, tuko hapa kupiga kura."

Chama tawala cha Waziri Mkuu Abiy Ahmed kimesimamisha wagombea wengi, na kinatarajiwa kushinda viti vingi bungeni.

Wafuasi wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed wakiwa katika mstari kuingia uwanjani huko Jimma Juni 16, 2021 ambako Waziri Mkuu alifanya kampeni yake kabla ya uchaguzi Juni 21, 2021.

Hata hivyo, kwa wapiga kura wengine kama vile Desa-lgn Shume, usalama ni muhimu zaidi.

Desalgn Shume, mkazi wa Addis Ababa anaeleza : “Jambo muhimu zaidi kwangu ni usalama. Tunahitaji serikali inayotuletea amani, umoja na ambayo itasimamisha mauaji kila mahali, na tunahitaji pia kuondolewa katika migawanyiko hii ya kikabila."

Waziri Mkuu Abiy, mwenye umri wa miaka 44, ambaye alishinda Tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2019 kwa kutekeleza mageuzi ya kidemokrasia na uchumi nchini Ethiopia, pamoja na makubaliano ya amani na nchi jirani ya Eritrea, alisema kura hiyo ni jaribio la kwanza la uchaguzi huru na wa haki nchini humo.

Lakini uchaguzi uligubikwa na hali ya kususiwa na vyama maarufu vya upinzani ambavyo vinakishutumu chama tawala kwa manyanyaso na vitisho na kuendelea kwa mzozo katika mkoa wa kaskazini wa Tigray ambapo wanajeshi wa serikali wamekuwa wakipambana na vikosi vya chama cha zamani cha mkoa huo tangu mwezi Novemba mwaka 2020.

Vita vimesababisha mzozo wa kibinadamu kwenye jimbo la Tigray na watu wapatao 350,000 wanakabiliwa na njaa kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Hakuna tarehe iliyowekwa ya kupiga kura katika eneo la Tigray, ambalo lina wawakilishi 38 wa bunge. Duru ya pili ya upigaji kura itafanyika mwezi Septemba, mwaka 2021.

Vyanzo vya habari mbalimbali ikiwa pamoja na AP, VOA News