Ethiopia : Chama cha Abiy Ahmed chapata ushindi mkubwa

Rais Sahle-Work Zewde

Rais Sahle-Work Zewde wa Ethiopa amepongeza kazi zilizofanywa na Tume ya Uchaguzi, NEBE, katika kutayarisha na kusimamia uchaguzi mkuu ambapo chama tawala cha Waziri Mkuu Abiy Ahmed kimepata ushindi mkubwa. 

Katika mkutano wa kusherehekea ushindi huo mjini Addis Ababa Rais Zewde amesema licha ya ukosefu wa amani katika baadhi ya sehemu za nchi, janga la COVID-19 na hali huko Tigray, kaskazini mwa nchi tume ya uchaguzi imefanya kazi kubwa ya ufanisi chini ya hali ngumu.

Kulingana na matokeo yaliyotolewa Jumamosi usiku chama cha Abiy cha Prosperity kimepata viti 410 kati ya 436 vya bunge.

Katika ujumbe wa Twitter Ahmed ameueleza uchaguzi kuwa ni wa kihistoria ambao anasema hivi sasa amepata mamlaka rasmi ya wananchi kutawala kwa miaka mitano.

Vyama vya upinzani na wagombea huru walipata viti vichache kabisa na duru ya pili ya uchaguzi inatarajiwa kufanyika katika wilaya 10 za uchaguzi.

Habari hii inatokana na vyanzo mbalimbali vya habari