COVID-19 yaenea kwa kasi Uturuki na Rashia, vifo vyaongezeka Marekani

Watu wakusanyika katika duka la bidhaa karibu na maeneo yao kununua bidhaa Ijumaa Aprili 10, 2020 baada ya amri ya kutotoka majumbani kwa siku mbili katika miji 31 kutangazwa mwisho ya wiki.

Idadi ya vifo kutokana na ugonjwa wa COVID-19 inaendelea kuongezeka Marekani na baadhi ya mataifa ya Ulaya yalioathirika zaidi na janga hilo huku ugonjwa huo ukienea kwa kasi Uturuki na Rashia.

Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani, WHO, Jumatatu kuna watu milioni 1,860,000 walioambukizwa na wengine takriban 115,000 waliofariki.

Marekani inakuwa nchi yenye idadi kubwa ya walioamukizwa pamoja na vifo hivi sasa ikiwa na watu zaidi ya 557,500 walioambukizwa na vifo 22,000. Huko Ulaya idadi ya maambukizi imefikia laki 880,000.

Wizara ya Afya ya Iran, nchi iliyoathirika zaidi huko Mashariki ya Kati, inaeleza kwamba idadi ya vifo imeongezeka kufikia 4,585 baada ya kutokea vifo 111 usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu pekee yake. Idadi ya walioambukizwa nchini humo imefikia elfu 73,303, ambapo watu elfu 45,983 wamepona kulingana na taarifa za wizara hiyo.

Korea Kaskazini na visiwa vya Comoro havijatangaza kuwepo na mtu yeyote aliyeambukizwa na virusi vya corona hadi hivi sasa.

Wakati huohuo barabara za mji mkuu wa Nigeria, Lagos, ambao kawaida kuna msongamano wa magari, hivi sasa zimefurika watu wakifanya mazoezi kutokana na kusitishwa shughuli zote katika juhudi za kupambana na ugonjwa wa COVID 19.

Mamia ya watu wamekuwa wakifanya mazoezi ya pamoja wakisema wanachukuwa kila tahadhari kutokaribiana ili kuzuia maambukizi.

Shughuli zimesitisha katika mji mkuu wa biashara wa Lagos, ambako ni kitovu cha ugonjwa huo nchini humo pamoja na mji mkuu wa Abuja na jimbo la Ogun. Serikali imeamrisha watu kubaki majumbani lakini watu wanasema afadhali kufanya mazoezi kuliko kukaa ndani bila ya kufanya chochote.