CDC : Ongezeko la maambukizi Marekani lawakumba wasiochanjwa

Rais Joe Biden

Marekani inashuhudia ongezeko katika maambukizi na vifo vya COVID-19, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kimeeleza Ijumaa.

CDC imesema maambukizi makubwa yanayotokana na aina mpya ya virusi vya Delta, yako miongoni mwa watu ambao kwa kiasi kikubwa hawakupokea chanjo.

Majimbo manne yenye viwango vya chini vya chanjo, yanahusika kwa asilimia 40 ya kesi mpya za wiki iliyopita.Lakini kesi zimeongezeka katika majimbo yote 50, maafisa wanasema.

Dkt Rochelle Walensky, mkurugenzi wa CDC, Marekani, alisema Ijumaa kwamba wiki iliyopita, Marekani ilikuwa na wastani wa maambukizi mapya kila siku ya watu 26,000. Alisema mlipuko huo umekuwa janga la wasiochoma chanjo.

Wakati huo huo, Rais wa Marekani Joe Biden, alirudia tathmini ya Walensky, akisema janga pekee tulilonalo, ni miongoni mwa wasiochoma chanjo.

Kundi la washauri wa kimataifa wa serikali, linasema wana wasiwasi kuhusu mipango ya Uingereza ya kuondoa karibu masharti yake yote ya janga hili ifikapo Jumatatu.

Washauri wanaamini kwamba hatua hiyo, itapelekea Uingereza kuingia katika aina mpya ya virusi vya Corona, na uwezekano wa kuifanya nchi kuwa sehemu inayosambaza mlipuko huo.

Habari hii inatokana na vyanzo mbalimbali