Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 17:19

Zimbabwe yakanusha nia ya kupeleka ndovu China


Ndovu kwenye mbuga ya kitaifa ya Mana, Zimbabwe
Ndovu kwenye mbuga ya kitaifa ya Mana, Zimbabwe

 Kundi moja la mazingira la Zimbabwe limeishitaki serikali kutokana na mpango wake wa kupeleka ndovu nchini China.

Kundi hilo Advocates4Earth, linailaumu China kwa kuweka ndovu kwenye mazingira hatari kiafya. Katika hati ya mashitaka iliowasilishwa mbele ya mahakama kuu, Advocates4Earth linaomba mamlaka ya kitaifa ya wanyama pori ya Zimbabwe izuiliwe kupeleka ndovu nchini China.

Lenin Tinashe Chisaira ambaye ni kiongozi wa Advocates4Earth anasema kuwa wanacho lenga ni kuomba mahakama itoe amri kwamba serikali ya Zimbabwe na wakala wake waheshimu sheria za kimataifa kwamba ndovu wa Afrika au wanyama wengine,wasipelekwe kwenye mataifa ambayo hayana mazingira asilia kwao.

Amesema kwamba wanahisi kuna baadhi ya idara za serikali zinazokusudia kukiuka kanuni hizo kwa kupeleka wanyama pori kwenye mataifa kama China bila kuzingatia mikakati ya kisheria. Mashitaka ya Advocated4Earth pia yanamjumuisha waziri wa mazingira ,Nqobizitha Mangalisi Ndlovu.

Idadi ya ndovu nchini Zimbabwe imeongezeka maradufu katika miaka ya karibuni na kufikia takriban laki moja, suala ambalo limesababisha baadhi ya wakulima kulalamika kuwa wanaharibu mimea pamoja na malisho ya mifugo yao.

Licha ya mashitaka yaliowasilishwa , idara ya kitaifa ya wanyamapori ya Zimbabwe imekanusha kwamba inapanga kupeleka ndovu China. Tinashe Farawo ambaye ni msemaji wa idara hiyo amesema kuwa hao ni watu wanaotafuta umaarufu, akiongeza kuwa kwenye hotuba ya Rais Emmerson Mnangagwa kwa taifa, alitoa onyo kwao watu wa aina hiyo.

Katika siku za nyuma, Zimbabwe imepeleka ndovu kwenye mataifa mengine licha ya malalamiko kutoka kwa wanaharakati wa haki za wanyama kama vile Advocates4Earth.

Alhamisi, maafisa wa China kwenye ubalozi wa taifa hilo mjini Harare hawakusema chochote ila kuwa hawakujumishwa kwenye kesi iliowasilishwa mahakamani.

Mtayarishaji : Harrison Kamau

XS
SM
MD
LG