Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 06, 2024 Local time: 02:34

Afrika yaiomba Benki ya Dunia kufadhili nafuu ya madeni yake


Moussa Faki Mahamat
Moussa Faki Mahamat

Viongozi wa Afrika wamekutana Alhamisi mjini Abidjan kujadili mipango mipya ya misaada na kuiomba Benki ya dunia kufadhili afueni yao ya kiuchumi na upatikanaji bora wa chanjo dhidi ya COVID-19.

Mkutano huo wa Abidjan nchini Ivory Coast unajiri wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kwamba, vifo vinavyohusishwa na virusi vya Corona vimeongezeka kwa asilimia 43 barani Afrika katika kipindi cha wiki moja, vikisababishwa na ukosefu wa vitanda kwenye vyumba vya huduma za dharura na oksijen.

WHO imesema kuongezeka kwa vifo kunalingana na ukosefu sugu wa chanjo, kuenea kwa aina mpya ya virusi vya Delta vinavyoambukiza kwa kasi, ambavyo sasa vimegundulika katika nchi 21 za Afrika, pamoja na watu kuchoshwa na hatua za kuzuia maambukizi.

Kando, baada ya mkutano na Benki ya dunia jana, viongozi wa Afrika waliomba dola billioni 100 katika ahadi za msaada wa kifedha mwishoni mwa mwaka kusaidia nchi zao kupata nafuu ya kujikwamua kwenye janga la COVID-19.

“Bado kuna mengi ya kufanya kumaliza mzozo huu,” amesema Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara ambaye alifungua mkutano huo wa Abidjan.

Rais Alassane Ouattara
Rais Alassane Ouattara

Ouattara ameeleza kuwa : “Bado kuna mengi ya kufanya kumaliza mzozo huu ambao, kama tunavyoona siku hizi limekuwa tatizo la ulimwengu lenye mizunguko kadhaa. Hakika, chini ya asilimia 3 ya raia wote wa Afrika ndio wamepokea dozi ya kwanza ya chanjo, ikilinganishwa na asilimia 54 Marekani na Umoja wa Ulaya.”

Moussa Faki Mahamat, mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika ametoa wito wa msaada wa kurekebisha deni la nchi za Afrika zilizo kwenye matatizo, ambazo zinakabiliwa “na mahitaji ya haraka ya pesa taslimu za kununua chanjo na kuweka misingi ya kufufua uchumi”.

Mahamat amefafanua ifuatavyo : “Hatutachoka kamwe kuomba marekebisho ya haraka ya deni yakiambatana na sera mbadala ambayo inakwenda zaidi ya haki maalum, ili kupunguza haja ya haraka ya pesa taslim kwa ajili ya ununuzi wa chanjo na kuweka misingi ya kufufua uchumi.”

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Felix Tshisekedi amesema janga la COVID-19 lilipelekea ukosefu wa ajira kuongezeka barani Afrika, ambapo kati ya watu millioni 25 na millioni 30 walipoteza ajira, huku wengine millioni 40 wakijikuta kwenye hali mbaya ya umaskini.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Rais Félix Tshisekedi
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Rais Félix Tshisekedi

Mkutano huo uliitishwa kujadili msaada wa Benki ya dunia kwa nchi za Afrika katika miaka mitatu ijayo.

Nicolas Kazadi, Waziri wa Fedha wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akizungumza kwa niaba ya nchi za Afrika ameziomba nchi fadhili kutekeleza ahadi zao.

Kazadi anaeleza : “Tunawasihi wafadhili wa taasisi ya IDA kuunga mkono mpango kabambe wa kuongeza uwezo kwa IDA ili kukusanya dola billioni 100 ifikapo mwishoni mwa 2021, kufikia malengo yaliyowekwa katika taarifa hii.”

Mazungumzo hayo yalisogezwa mbele kwa mwaka mmoja kusaidia nchi maskini kukabiliana na athari za janga la Corona.

Katika miaka mitatu iliyopita, taasisi ya fedha ya Benki ya Dunia, IDA, ilitenga dola billioni 22 kila mwaka kwa wastani.

Kati ya nchi 76 zilizofaidika na msaada huo wa IDA, 39 ziko Afrika.

Mwezi Mei, jumuia ya kimataifa iliahidi katika mkutano mjini Paris, kuisaidia Afrika kupambana na janga la Corona, lakini haikutangaza kiwango cha pesa itakazotoa.

Chanzo cha Habari : AFP

XS
SM
MD
LG