Afisa mkuu wa jeshi la Burundi aliliambia shirika la habari la AFP kwamba wanajeshi hao walikuwa tayari kuungana na wenzao wa nchi zingine za kikanda, katika operesheni hiyo.
Baadhi ya mataifa saba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yalituma wanajeshi mwishoni mwa mwaka jana mashariki mwa DRC, eneo ambalo limekuwa likipambana na kuongezeka kwa wanamgambo, wakiwemo waasi wa M23.
Mapigano katika jimbo la Kivu Kaskazini yamesababisha idadi kubwa ya watu kuyahama makazi yao na kuzidisha mivutano ya kikanda, huku serikali ya DRC ikiishutumu Rwanda kwa kuunga mkono M23 -- madai yaliyokanushwa na Kigali lakini yanaungwa mkono na Marekani na mataifa kadhaa ya Magharibi.
Wanamgambo hao waliibuka tena mwishoni mwa 2021, na baadaye kumiliki maeneo mengi ya Kivu Kaskazini, ikiwa ni pamoja na eneo kubwa la kaskazini mwa mji mkuu wake Goma.
EAC, ambayo imefanya mikutano kadhaa kusuluhisha mzozo huo na kutoa wito wa kuondolewa kwa M23 kutoka maeneo yaliyokaliwa, iliunda kikosi cha kikanda kinacholenga kuleta utulivu mashariki mwa DRC.
Lakini maelfu ya watu waliandamana mjini Goma mwezi uliopita, wakishutumu jeshi la EAC kwa kutokuwa na msimamo mbele ya makundi yenye silaha.
Siku ya Ijumaa, afisa mkuu wa jeshi la Burundi aliiambia AFP "kikosi cha takriban wanajeshi 100 kitasafiri kesho kuelekea Goma".