Vyombo vya habari vya Uganda vinaripoti kwamba mkutano wa wakuu wa jeshi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana kwamba wanajeshi wa Uganda watashika doria katika sehemu za Bunagana, Kiwanja/Rutshuru na Mabenga.
Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waliamuru waasi wa M23 kuacha vita na kukumbatia mchakato wa kisiasa wa kuleta amani nchini DRC.
Waasi hao hata hivyo wamekataa ushauri huo na kuendelea kupigana na wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wakuu wa majeshi wa nchi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki walikubaliana kwamba ni lazima waasi wa M23 waondoke Rutshuru, Kiwanja na Bunagana ifikapo Machi 30, 2023.
Kulingana na vyombo vya habari vya Uganda, wanajeshi wa Uganda wataingia DRC kwa ajili ya kupambana na M23, ifikapo mwishoni mwa mwezi wa Februari.
Naibu wa kamanda wa UPDF na mtoto wa Museveni wana msimamo tofauti kuhusu M23
Naibu wa mkuu wa majeshi wa Uganda Luteni Jenerali Peter Elwelu alisema mwaka uliopita kwamba “Kupeleka wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni hatua nzuri na haiwezi kuchukua zaidi ya saa 24 kwa jeshi la jumuiya kuwamaliza nguvu waasi wa M23”.
Elwelu alisisitiza kwamba waasi wa M23 “wanajua hilo vizuri sana.”
Lakini mshauri wa rais Yoweri Museveni kuhusu operesheni maalum, ambaye pia ni mtoto wa Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, aliandika ujumbe wa Twitter akisema kwamba “Jeshi la UPDF litaingia DRC kulinda raia na wala sio kupigana na waasi wa M23”, akiongezea kwamba wanajeshi wa UPDF watakuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba mradi wa kujenga barabara unaotekelezwa na Uganda ndani ya DRC unakamilika.
“Tutafanya kazi na ndugu zetu wa DRC na Rwanda kuhakikisha kwamba kuna usalama,” alisema Muhoozi katika ujumbe wa Twitter.
Shughuli kwenye mpaka wa Bunagana kati ya Uganda na DRC
Biashara kati ya Uganda na DRC inatarajiwa kuongezeka iwapo waasi wa M23 wanaondoka kwenye mpaka wa Bunagana.
Biashara kati ya nchi hizo mbizi zilisitishwa mnamo Juni 2022, kupitia mpaka wa Bunagana, baada ya waasi wa M23 kuuteka mji huo.
DRC yenye jumla ya watu milioni 107, ni soko kubwa kwa nchi za Afrika Mashariki.
Mnamo Januari 2022, Uganda iliripoti kupata kiasi cha dola milioni 71 kutokana na biashara kati yake na DRC.
Idadi kubwa ya bidhaa kutoka Uganda kuelekea DRC zinapitia mpaka wa Bunagana.
DRC inanunua saruji na vifaa vingine vya ujenzi kutoka Uganda.
Bidhaa nyingine ni mafuta ya kupikia na pombe.
Kwa jumla, Uganda ilipata dola milioni 100 kutoka kwa uuzaji wa saruji, mafuta ya kupika na pombe kutokana na biashara yake na DRC. Biashara hiyo imesimama kwa sasa.
Uganda ilikuwa inajenga barabara ndani ya DRC kwa ajili ya kurahihisha biashara. Ujenzi huo vile vile umesitishwa. Barabara hiyo ni ya umbali wa kilomita 223.
Namna wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamegawana kazi
Kulingana na makubaliano ya wakuu wa jeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanajeshi wa Burundi watashika doria katika sehemu za Kirolirwe na Kitchanga.
Mapigano makali kati ya waasi wa M23 na wanajeshi wa serikali yanaendelea katika sehemu hizo.
Mji wa Sake unapatikana kilomita 15 kutoka mji wa Goma.
Waasi wa M23 wamekuwa na lengo kubwa la kuuteka mji wa Goma lakini wamekosa mafanikio.
Wanajeshi wa Kenya watashika doria katika sehemu za Kibumba, Rumangabo, Tongo, Bwiza na Kishishe
Wanajeshi wa Sudan kusini wamepangiwa kushika doria katika sehemu za Rumangabo na kushirikiana na wanajeshi wa Kenya.
Tanzania haishiriki katika mpangilio wa kutuma wanajeshi chini ya jumuiya ya Afrika mashariki.
DRC ilikataa wanajeshi wa Rwanda kuingia nchini humo.
Wanajeshi wawili wa Rwanda ambao walikuwa wameruhusiwa kufuatilia operesheni hiyo walifukuzwa na serikali ya DRC.
Mvutano kati ya DRC na Rwanda
Serikali ya DRC inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23.
Ripoti ya wataalam wa Umoja wa Mataifa imesema kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi hao.
Picha za satallaiti za Umoja wa Mataifa ambazo zimechapishwa na mashirika kadhaa ya vyombo vya habari vya kimataifa zinaonyesha picha za wanajeshi wanaodaiwa kuwa wa Rwanda wakivuka mpaka na kuingia DRC.
Rwanda imekanusha madai yote dhidi yake na badala yake inasema kwamba DRC inawaunga mkono waasi wa FDLR wenye nia ya kuuangusha utawala wa rais Paul Kagame.