Bunge la Uturuki kupiga kura kuridhia Sweden kujiunga rasmi na NATO

NATO

Bunge la Uturuki leo Jumanne litaidhinisha Sweden kuingia katika muungano wa NATO Baada ya kucheleweshwa kwa hatua hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Uamuzi huo unakuja baada ya tume inayohusika na Mambo ya Nje ya Uturuki kuidhinisha ombi la nchi hiyo kuwa mwanachama mwezi uliopita.

Mnamo 2022, Sweden na Finland zilituma maombi ya kutaka kuwa wanachama wa muungano huo. Na ingawa Finland hatimaye ilijiunga NATO mwezi Aprili 2023, Uturuki ilikataa kuidhinisha ombi la Sweden, uamuzi ambao umekatisha tamaa washirika wake wa Magharibi.

Hapo awali, Uturuki ilikataa kuidhinisha uanachama wa Sweden kwa madai kwamba nchi hiyo iliunga mkono wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK), ambacho kinatambuliwa kama kundi la kigaidi na Uturuki, Umoja wa Ulaya na Marekani.

Tangu wakati huo Sweden imeandaa mswada wa kupambana na ugaidi unaofanya uanachama wa kundi lolote la kigaidi kuwa kinyume cha sheria.