Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken yuko Berlin kwa mazungumzo Jumatano na viongozi wa Ujerumani na kushiriki katika mkutano kuhusu mustakabali wa kisiasa wa Libya.
Tuna nafasi ambayo hatukuwa nayo katika miaka ya hivi karibuni kusaidia Libya kwa hali ya juu ili kusonga mbele kama nchi salama na huru " Blinken alisema baada ya mkutano wa asubuhi na Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas.
Ujerumani na Umoja wa Mataifa wanaandaa mkutano wa Berlin, wakitafuta kuimarisha juhudi za hapo awali za kusitisha mapigano nchini Libya na kuunga mkono serikali thabiti.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa pamoja na Maas, Blinken alisema kulikuwa na makubaliano juu ya hatua gani bora za kuchukua kuisaidia Libya, haswa kuhakikisha utekelezaji wa kusitisha mapigano na kuondoka kwa vikosi vya kigeni kutoka nchi hiyo.
Mjumbe Maalum wa Marekani kwa Libya Richard Norland aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu kwamba mkutano huo utatoa kasi kwa hatua ambazo zinahitaji kuchukuliwa mapema kwa ajili ya uchaguzi utakaofanyika Desemba, ikiwa ni pamoja na kuanzisha msingi wa kikatiba na kisheria wa kupiga kura.