Wanawake hao wajasriamali wamekutana leo jijini Dar es Salaam baada ya kuhitimu mafunzo ya takribani wiki 14 yenye lengo la kuwapa elimu juu ya matumizi ya teknolojia katika kukuza biashara zao pamoja na kuwapa fursa za masoko katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Sharon Akanyana ambaye ni miongoni mwa wanufufaika wa program ya AWE kutoka nchini Rwanda amesema jukwaa hilo limeweza kuwapa mafunzo wanawake hao ya jinsi ya kuendesha na kusimamia biashra zao, kusimamia raslimali watu pamoja na fedha suala ambalo limepelekea wao kama wajasriamali wadogo kukua.
“na nimefaidika kama mjasiriamali katika programu haswa nilipenda programu ya kujenga ndoto ambayo ni programu ya mtandaoni ambayo inatufundisha mambo ya msingi ya kuendesha biashara usimamizi wa rasilimali watu, usimamizi wa fedha, utunzaji wa vitabu, ni vitu vya msingi sana vinavyosaidia. wewe kama mfanyabiashara mdogo kukua” alisema Akanyana.
Licha ya programu ya AWE kuwakutanisha wajasriamali na wafanyabiashara vilevile imeweza kuwasaidia wanawake wenye malengo ya kufungua makampuni na taasisi mbali mbali kwa kuwapa mafunzo sahihi ya namna ya kuanzisha taasisi na makampuni.
Akizungumza na sauti ya Amerika Aslatu Nguku ambae ni muanzilishi wa kampuni na taasisi ya Mama Health iliyopo Dodoma amesema programu ya AWE imemjengea uwezo wa kujiamini na hata kuifikia serikali hivyo kupelekea taasisi yake kukua kwa kiwango kikubwa.
Na kusema kuwa “AWE ilinisaidia kwanza ilinijengea ujasiri wakufanya nakupitia yale mafunzo ya AWE niliweza kutoka na kuwafuata watu wengine hasa serikali kwasababu nilikuwa nafanya tu kama mjasiriamali mdogo lakini nimeweza sasa kupitia yale mafunzo yao nguvu zao nimeweza sasa kuwafuata serikali kwenye zile taasisi husika nimeweza kwenda nao lakini pia nimeweza kufanya masuala yote ya mahesabu ambayo wanafundisha.”
Naye balozi wa Marekani nchini Tanzania Michael Battle alisema kuna umuhimu mkubwa kwa wajasriamali wanawake kukutana na kupeana elimu juu ya masuala ya kijasiriamali ili kumaliza umasikini katika ukanda huo ya wa Afrika mashariki.
Balozi huyo wa Marekani alisema,“ni muhimu kwa wanawake wajasiriamali kupata nafasi ya kuungana kwa pamoja na njia pekee ya kumaliza umaskini katika Afrika Mashariki ni kuwa na wanawake wenye nguvu sana ambao wanajihusisha na biashara zinazoungwa mkono na taifa lao na kuungwa mkono na wanaume wa taifa lao pia hii inaleta tofauti katika kupanda kwa mtu binafsi na inafanya tofauti katika kukua kwa taifa.”
Hata hivyo mkufunzi na mjasiriamali Victoria kisyombe, alimalizia kwa kusisitiza nchi za Afrika kutambua umuhimu wa mwanamke kushiriki katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi kwani kumuendeleza mwanamke ni kuendeleza familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Imetayaraishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika, Dar es salaam.