Afisa polisi afunguliwa shtaka la kumuua bila ya kukusudia Mmarekani Mweusi

Kim Potter

Afisa wa polisi wa zamani, jimbo la Minnesota Alhamisi atafikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani kwa shtaka la kumuua bila ya kukusudia kijana Mmarekani Mweusi Daunte Wright, wakati aliposimamishwa akiwa ndani ya gari yake.

Mwendesha mashtaka wa kaunti ya Washington Pete Orput alitangaza Jumatano shtaka hilo dhidi ya Kim Potter.

Tukio hilo la mauaji lilitokea katika kaunti ya Hennepin, lakini kwa mujibu wa sera iliyopitishwa mwaka 2020 katika jimbo la Minnesota, kesi imepelekwa kwenye kaunti nyingine ili kuepuka mgongano wa maslahi.

Maandamano yamekuwa yakifanyika kila siku tangu Wright auwawe kwa kupigwa risasi siku ya Jumapili, yakifanyika hasa mbele ya makao makuu ya polisi katika eneo la Brooklyn Center, mjini Minneapolis, huku waandamanaji wakiomba haki itendeke kwa kifo cha Daunte Wright.

Afisa huyo wa zamani Kim Potter na mkuu wa polisi Tim Gannon wote walijiuzulu kutoka idara ya polisi ya Brooklyn Center baada ya mauaji ya Wright.