Abdi Hashi Abdullahi achaguliwa tena kuwa Spika wa Bunge la Somalia

FILE - Spika wa Bunge la Somalia, Abdi Hashi Abdullahi.

Spika wa Bunge la Somalia Abdi Hashi Abdullahi amechaguliwa tena katika mji mkuu wa Mogadishu Jumanne. 

Abdulahi alishikilia uongozi wa Bunge la Juu lenye viti 54 baada ya kupata kura 28 wakati mpinzani wake wa karibu Salah Jama alipata kura 24 na mpinzani wa pili Osman Dubbe alipata kura mbili tu.

Uteuzi wa Abdulahi unaiweka nchi kukaribia kufanya uchaguzi wake mkuu wa kumchagua rais kuliongoza taifa hilo la Pembe ya Afrika kwa kipindi cha miaka mitano.

Hata hivyo hii itakuwa ni baada ya kuchagua spika wa Bunge la Chini lenye wajumbe 275, ambalo lina nguvu na ushawishi nchini Somalia.

Bunge la chini pia limepangiwa kufanya uchaguzi wa spika na wasaidizi wawili Jumatano, kwa mujibu wa televisheni ya ndani ya CBA.

Nchi hiyo imeshindwa kufanya chaguzi kadhaa zilizopangwa hali iliyosababisha kuwekewa vikwazo na marekani kwa wabunge.