Bunge jipya la Somalia limekutana kwa mara ya kwanza Jumamosi katika kile kinachoelezewa ni hatua muhimu kuelekea kukamilisha mchakato wa kumteua rais mpya.
Wasomali huwa hawapigi kura moja kwa moja kuwachagua wawakilishi wao au rais katika taifa hilo linalokumbwa na vita.
Bali uchaguzi nchini Somalia hufuata utaratibu wa kutatanisha, ambapo wajumbe wa mabunge ya majimbo na wajumbe wa koo huwateua wabunge wa baraza kuu la bunge la taifa ambao nao humteua rais.
Karibu wabunge 300 waliapishwa siku ya Alhamisi zaidi ya mwaka mmoja tangu muda wao kumalizika kufuatia utaratibu wa upigaji kura uliogubikwa na vurugu na kuhujumiwa na ghasia zilizosababisha vifo vingi pamoja na mivutano ya madaraka kati ya rais wa hivi sasa na waziri mkuu.
Kikao cha ufunguzi Jumamosi kilianzisha utaratibu wa kuwachagua maspika wa baraza kuu na baraza dogo la bunge kabla ya kuanza majadiliano ya kumteua rais mpya.
Tarehe ya kumchagua rais haijapangwa bado.
Uchaguzi wa bunge ulitakiwa kukamilika kabla ya muhula wa Rais Mohamed Abdullah Mohamed kumalizika Februari 2021.
Lakini ugomvi wa kisiasa ulikwamisha utaratibu na muda wa muhula wa rais ukamalizika bila ya kufikia makubaliano.
Rais Mohamed anayefahamika zaidi kama Farmaajo, alijaribu kuongeza muda wa utawala wake kupitia amri ya kiutendaji, lakini alikabiliwa na upinzani mkali na maandamano ya upinzani mjini Mogadishu ambapo makundi ya kisiasa yanayopingana yalipigana barabarani.
Kutokana na shinikizo la Jumuia ya Kimataifa, rais alimteua waziri mkuu Mohamed Hussein Roble ili kuweza kufikia maridhiano na kusonga mbele, lakini wanasiasa hao wawili hawakukubaliana juu ya mambo mengi na kukwamisha utaratibu.
Ugomvi mkubwa kati ya Roble na Farmaajo ulizusha hofu ya kuzidisha mivutano katika taifa hilo la pembe ya Afrika linalopambana na uasi wa karibu muongo mmoja kutoka kwa wanamgambo wa kiislamu na tishio la njaa.