Asasi hizo zimeiita kauli hiyo ya mkuu wa mkuu wa mkoa kuwa ni kinyume na sera ya elimu na inaendelea kumdidimiza mtoto wa kike katika kuyafikia malengo yake.
Mkuu wa mkoa huyo wa Singida aliitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wilayani Itigi ambapo alieleza jinsi alivyojiandaa kushughulikia na kukomesha tatizo la mimba za utotoni wilayani humo.
Wakili Anna Henga, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam akizungumzia kauli hiyo ameelezea masikitiko yake kwa vile yanarudisha nyuma jitihada za kutetea haki za watoto na kuendelea kudidimiza haki za wanawake.
Alisema “Kupata uja uzito sio kosa la jinai lakini pia hawa watoto wanaposema kwamba watachukuliwa hatua ni hatua zipi na kwa sheria ipi. Mimi kama mwanasheria najua hakuna sheria inayomuadhibu huyu mtoto kwa kupata uja uzito”
“Kwahiyo mimi naona hii kauli ni ya kuzidi kudidimiza haki za wanawake na kudidimiza watoto wa kike na kama tunatafuta marais wengine wengi wa kike kama Samia itakuwa ngumu kuwapata,” aliongeza
Henga amesema kuwa kauli hiyo inapingana moja kwa moja na Sera ya elimu ya serikali ambapo kwa mujibu wa waraka namba mbili wa mwaka 2021 umetoa ruhusa kwa watoto wa kike wanaopata ujauzito wanapokuwa shule kurejea kuendelea na masomo miaka miwili baada ya kujifungua.
Naye Annastazia Ruggaba, Mkurugenzi wa Idara ya Utetezi katika Taasisi ya Twaweza Afrika Mashariki, amesema kuwa mamlaka za juu zinapaswa kumchukulia hatua Mkuu wa Mkoa huyo kwa kwenda kinyume na kauli za viongozi wake. Hii ni baada ya Rais Samia Suluhu Hasan kutoa msimamo wake juu ya masuala ya watoto wa kike kupata ujauzito baada ya kuingia madarakani.
“Kwanza angepaswa achukuliwe hatua na uongozi wa juu kwasababu mheshimiwa Rais alishatoa msimamo wake na wizara husika ilishatoa msimamo wao” alisema.
Na kuongeza kuwa “Yeye ni nani anakuja kupingana na msimamo wa mheshimiwa Rais? Kwahiyo, angepaswa achukuliwe hatua kwasababu anarudisha nyuma jitihada za kumkomboa mtoto wa kike ambaye kimsingi ana vikwazo vingi sana kuweza kufikia elimu yake”
Hata hivyo Mratibu wa mtandao wa haki za binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Ole Ngurumwa amesema kauli hiyo inaweza ikatumika kama kitisho kwa wale wanaofanya vitendo ambavyo vinapelekea kusababisha mimba za utotoni na kusaidia kupunguza changamoto ya mimba za utotoni katika maeneo mengi ya nchi.
“Ni kauli ambayo pengine imezungumzwa tu kama kiongozi kwa lengo la kutishia au kwa lengo la kutaka watoto na wazazi wakati mwingine wawe makini na hii inaweza ikasaidia wakati mwingine wale ambao walikuwa wanalegalega wakisikia kauli kama hiyo inaweza ikawafanya wakawa makini na kupunguza idadi ya watoto wanaopata mimba wakiwa shule,” alisema Ngurumwa.
Nalo Jukwaa la elimu kwa mtoto wa kike Tanzania limewahimiza viongozi na wadau kuzingatia na kuheshimu sheria na miongozo iliyowekwa kuhusu ulinzi na usalama wa mtoto. Limeonya dhidi ya kusimamia misimamo binafsi, kwa kuwa Tanzania inaongozwa na sheria.
Imetayarishwa na Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika, Dar es Salaam