Takriban watu 12 waliuawa na zaidi ya 50 bado hawajulikani walipo, baada ya mvua kubwa kusababisha maporomoko ya ardhi kwenye mto kusini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, afisa wa eneo hilo, na kiongozi wa shirika la kiraia walisema Jumapili.
Maporomoko hayo yalitokea Jumamosi adhuhuri katika wilaya ya Dibaya Lubwe katika jimbo la Kwilu, na kusababisha udongo na uchafu kwenye ukingo wa Mto Kasai, ambapo boti moja ilikuwa ikitia nanga, na watu walikuwa wakifua nguo.
Kaimu gavana wa jimbo hilo Felicien Kiway alisema, miili 12 imetolewa kutoka kwenye vifusi hadi sasa, ikiwa ni pamoja na wanawake tisa, wanaume watatu na mtoto mchanga.
Mratibu wa jumuiya ya kiraia ya eneo hilo, Arsene Kasiama, alisema udongo huo uliwaangukia watu waliokuwa wakinunua bidhaa sokoni.