Darzeni wafariki katika mapigano mabaya kuwahi kutokea Libya 2023

Moshi ulioenea angani kufuatia mapigano kati ya makundi mawili yenye nguvu mjini Tripoli, Libya, Aug. 15, 2023.

Makundi mawili yenye nguvu yalipambana katika mji mkuu wa Libya siku ya Jumanne ikiwa ni ghasia mbaya sana kuwahi kutokea mwaka huu.

Lakini mapambano hayo yaliyosababisha vifo yametulia baada ya upande mmoja kumuachia kamanda ambaye alikuwa kizuizini hatua ambayo awali ilichochea mapigano hayo.

Idara ya afya ya Tripoli ilisema watu 27 waliuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa katika ghasia, bila ya kusema kama idadi inajumuisha wote wapiganaji na raia.

Kikosi maalum cha kijeshi na Birgedi ya 444 ni makundi mawili ya kijeshi yenye nguvu mjini Tripoli na mapigano yao yaliyoanza Jumatatu yalitikisa wilaya zote katika mji mkuu.

Moshi mweusi ulizagaa katika baadhi ya maeneo ya mji huo sehemu kubwa ya siku ya Jumanne, na milio ya silaha nzito ilitikisa kote mitaani wakati mapigano yalipozuka katika maeneo mbalimbali.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters.