Serikali ya Waziri Mkuu Kallas ni kati ya zile zinazounga mkono kwa dhati nchi ya Ukraine, katika eneo hilo.
Wachambuzi wa kisiasa wanasema Kallas na chama chake huenda wakaibuka washindi dhidi ya Martin Helme na chama cha mrengo mkali wa kulia cha EKRE.
Kallas ameahidi kushabikia mchakato wa kuiwezesha Estonia kutumia nishati zaidi ya kijani na kuendelea kuwapokea wakimbizi wa Ukraine.
Wakati huo huo, Helme amewaambia wafuasi wake kwamba ushindi wa EKRE utasimamisha mpito wa nishati ya kijani na kusitisha mtiririko wa wakimbizi kutoka Ukraine.
Viongozi wote wawili wamesema wanatazamia kuongoza serikali ijayo ya mseto.
Takriban nusu ya wapiga kura wanaotimiza masharti ya kupiga kura nchini Estonia tayari walikuwa wamepiga kura zao kwa njia ya kielektroniki.
Estonia ilijitenga na Umoja wa Kisovieti mwaka wa 1991 na imefuata mwelekeo wa mataifa ya Magharibi, ikijiunga na NATO na Umoja wa Ulaya.