Vifo kutokana na Covid duniani vyapungua zaidi tangu janga kuanza - WHO

PICHA YA MAKTABA: Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO,  anasema idadi ya vifo vilivyotokana na Covid 19 wiki iliyopita ilikuwa ndiyo ndogo zaidi iliyoripotiwa katika janga hilo tangu mwezi Machi  mwaka 2020.

Hali hiyo inaashiria kile kinachoweza kuwa hatua ya mabadiliko katika mlipuko huo wa miaka kadhaa, kwa mujibu wa shirika la habari la AP.

Katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema dunia haijawahi kuwa katika nafasi nzuri ya kukomesha COVID-19, kuliko wakati huu.

Katika ripoti yake ya kila wiki kuhusu janga hilo, shirika la afya la Umoja wa Mataifa lilisema vifo vilipungua kwa asili mia 22, katika wiki iliyopita.

Takriban vifo vya watu 11,000 viliyoripotiwa duniani kote.

Hata hivyo, WHO ilionya kuwa kulegea kwa juhudi za upimaji na ufuatiliaji kunamaanisha kuwa visa vingi vya Covid 19 haviripotiwi.