Wakati Waukraine wakikimbia vita, taarifa za ubaguzi dhidi ya Waafrika zaibuka

Waafrika wakazi Ukraine wakisubiri katika kituo cha treni cha Lviv, Jumapili, Feb. 27, 2022, Lviv, west Ukraine. (AP Photo/Bernat Armangue)

Wafanyakazi na wanafunzi wa Kiafrika wanaohangaika kukimbia Ukraine wakati nchi hiyo imekabiliwa na uvamizi wa Russia wanalalamika kuzuiliwa kupanda mabasi, treni na pia kuvuka mipaka huku kipaumbele kikitolewa kwa raia wa Ukraine.

Mwandishi wa VOA huko magharibi mwa Ukraine anasema kwamba kipaumbele kinatolewa kwa raia wa Ukraine lakini hajaona ushahidi wa Waafrika kutendewa tofauti na raia wengine wa kigeni.

Hata hivyo, baadhi ya Waafrika – wakiwemo maelfu ya watu waliokata tamaa wanaojaribu kuondoka Ukraine – wanadai ubaguzi wa rangi, madai ambayo yamekanushwa vikali na mamlaka za Ukraine na kuwepo wasiwasi kutoka Marekani na taasisi za kimataifa.

Augustine Akoi Kollie, raia wa Liberia anayasomea udaktari magharibi mwa Ukraine katika mji wa Ternopil, alisema alishuhudia tofauti fulani wakati alipokuwa akisubiri usiku wa Jumamosi kwenye eneo la mpakani kribu na Suceava, nchini Romania.

Watu walikuwa wamesimama katika mistari mirefu wakitetemeka kwa baridi, wakikumbatia mizigo yao na watoto wao, na “kama akitokea raia wa Ukraine, unatakiwa hama na kuwapisha Waukraine waende mbele ya mstari,” Kollie ameiambia VOA. Japokuwa mamlaka ziliwaita wanawake na watoto kushughulikiwa kwanza, wanawake wa Kiafrika waliachwa nyuma, amesema.

Jengo lililoharibiwa na shambulizi la mabomu yaliyopigwa na majeshi ya Russia katika mji wa pili kwa ukubwa Kharkiv Machi 3, 2022.(Photo by Sergey BOBOK / AFP)

“Ni ubaguzi wa rangi,”alisema, “kwa sababu kama unasema unawachukua wanawake na watoto, unao wanafunzi wa kigeni ambao ni wanawake. Hivyo kwa nini huwachukui na wao?”

Kollie pia ameona tabia za ushari, ambapo mmoja wa wasafiri wenzake walirekodi katika picha ya video wakati wakisubiri mpakani. Video hiyo, ambayo VOA pia iliipata, inaonyesha tukio la wakati wa usiku la wanaume waliovalia unifomu wakiwachukua kile alichokieleza Kollie “wanafunzi wa kigeni,” ambao walikuwa wamekaa chini na hawaonekani nyuma ya gari iliyokuwa imeegeshwa. Watu hao walipiga risasi kadhaa hewani.

Maelezo yake yanalingana na ripoti za vyombo vya habari nyingine.

Daktari Mnigeria mwenye umri wa miaka 24 ameliambia gazeti la The New York Times alikuwa amekwama kwa zaidi ya siku mbili katika mpaka wa Ukraine na Poland katika mji mpaka wa Medyka, nchini Poland huku walinzi wakiwazuia wageni na kuruhusu Waukraine kuvuka.

“Walikuwa wanawapiga watu kwa fimbo,” daktari huyo, Chineye Mbagwu, ameliambia The Times. “Waliwapiga makofi, na kuwapiga na kuwasukuma nyuma kabisa ya mstari. Ilikuwa mbaya sana.”

Hashtag #AfricansinUkraine imekuwa ikivuma kwenye Twitter, ikionyesha picha za video za watu Weusi wakionekana wanazuiliwa kupanda treni au kuondolewa katika nafasi zao za kukaa. VOA haijaweza kuthibitisha video hizo yenyewe kutumia vyanzo vyake.

Mwandishi wa VOA akiripoti kutoka Ukraine amesema mamlaka huko zimetoa kipaumbele kwa Waukraine kuondoka na mabasi na treni, na kufanya iwe vigumu kwa wageni – ikiwemo yeye, mzungu raia wa Ulaya – kuondoka.

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba, alituma ujumbe wa Tweet Jumanne: “Uvamizi wa Russia huko Ukraine umewaathiri Waukraine na raia wengine katika njia nyingi zenye kuvunja moyo. Waafrika wanaotaka kuondolewa ni rafiki zetu na wanatakiwa kupata fursa sawa sawa kuweza kurejea makwao salama. Serikali ya Ukraine inatumia kila juhudi kutatua tatizo hili.

Habari zinazo kera

Umoja wa Afrika umetoa taarifa Jumatatu ukisema maafisa wake wa ngazi ya juu – mwenyekiti wa hivi sasa Macky Sall, rais wa Senegal, na Moussa Faki Mahamat, mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika – “walikerwa hasa na taarifa kuwa raia wa Afrika upande wa mpaka wa Ukraine wananyimwa haki yao ya kuvuka mpaka kuelekea eneo lililokuwa salama.

Moussa Faki Mahamat

“Ripoti kuwa Waafrika wametengwa na kutendewa mambo yasiyokubalika yatakuwa ni ubaguzi unaoshtusha na uvunjifu wa sheria za kimataifa,” taarifa hiyo imeeleza.

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu haikuweza kuthibitisha ripoti hizo, “lakini zinakera,” shirika hilo limesema katika barua pepe iliyotumwa kwa VOA Jumanne. “Kupita kwa salama na uwezo wa kutafuta sehemu salama ni haki ya kila mtu aliyeathiriwa na vita.” ICRC inafanya kazi na kuitikia mahitaji ya kila mtu aliyeathiriwa na vita.”

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imelaani majaribio yoyote ya ubaguzi.

“Tunafahamu kuhusu hizi ripoti za vyombo vya habari,” msemaji wa wizara amesema Jumatatu. “ Kitendo chochote cha ubaguzi wa rangi, hususan katika hali ya mgogoro, hali sameheki.”

Msemaji huyo wa wizara hiyo ilikuwa “ikiwasiliana karibu na mashirika ya UN yaliyoko nchini humo kuhakikisha kuwa kila mtu anayevuka kwenda nchi hizo jirani anapokelewa bila kubaguliwa na kupewa hifadhi inayostahili kama mazingira yanavyotaka.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken

Wakati huo huo, AU imepongeza juhudi za nchi wanachama na balozi mbali mbali katika nchi jirani kuwapokea raia wa Afrika na familia zao waliokuwa wanajaribu kuondoka Ukraine.

Balozi wa Nigeria nchini Romania, Safiya Ahmad Nuhu, ameiambia Idhaa ya Hausa ya VOA kuwa zaidi ya Wanigeria 600 wamewasili Bucharest “na kuna wengine zaidi ndani ya mabasi ambao wanakuja kutoka sehemu mbalimbali za mpakani.”

“Mamlaka nchini Romania walikuwa wasaidifu katika kuratibu, kuandaa na msaada,” amesema. Siyo tu kwamba inahusisha serikali lakini hata watu, taasisi, vyuo vikuu, watu binafsi – wote wamekuwa wasaidifu katika kutoa misaada.”

Kollie, mwanafunzi raia wa Liberia, alisema wakati fulani yeye na wenzake wawili walivuka kuingia Romania, walipewa mablanketi, chakula kingi na usafiri kuelekea mji wa Timisoara, ambako wanaishi pamoja katika chumba cha hoteli. Alisema watu wapya wanaowasili waliambiwa watapata msaada wa chakula na malazi kwa siku 30.

Inatarajiwa kuongezeka kwa wakimbizi

Umoja wa Mataifa unatarajia kuwa, kutokana na mashambulizi mfululizo yanayofanywa na Russia, wakimbizi wataendelea kumiminika kuvuka mipaka ya Ukraine.

“Sikuwahi kushuhudia kiwango cha kustaajabisha cha ongezeko la watu wanaokimbia vita,” huku idadi “ikiongezeka kila saa haraka kuanzia Alhamisi,” amesema Kamishna wa UN anayesimamia Wakimbizi Filippo Grandi, akihutubia Baraza la Usalama la UN Jumatatu. “… Hivi sasa tunapanga kuwashughulikia wakimbizi wapatao milioni 4 katika siku na wiki zijazo. Ongezeko hili la haraka la wakimbizi litakuwa na mzigo mkubwa kwa nchi zinazowapokea.”

Tayari, ongezeko la wanaoondoka linawakilisha idadi kubwa zaidi ya wale waliolazimika kukimbilia Ulaya tangu vita vya Balkan mwanzoni mwa miaka ya 1990, Grandi alisema. Wakati huo, zaidi ya watu milioni 2 walikimbia makazi yao, shirika la wakimbizi la UN lilikadiria wakati huo.

Filippo Grandi

Grandi ameeleza kuwa katikati ya mgogoro unaoendelea, zaidi ya watu 280,000 wameomba msaada nchini Poland; nchini Hungary, 94,000; huko Moldova, takriban 40,000; huko Slovakia, 30,000 – pamoja na maelfu sehemu nyingine Ulaya. Grandi alisema “idadi kubwa” pia imeelekea kutafuta hifadhi katika Shirikisho la Russia.

Tume ya Ulaya – mhimili wa Serikali ya Umoja wa Ulaya – mapema wiki hii ilijadili ikiwataka nchi wanachama kutoa hifadhi ya muda kwa Waukraine hadi miaka mitatu. Gazeti la New York Times na Reuters wameripoti. Wakazi wa Ukraine, ambao siku ya Jumatatu waliomba uanachama wa EU, hivi sasa wanaweza kukaa hadi siku 90 na kusafiri bila visa katika nchi hizo za umoja huo.

Alipoulizwa na VOA kuhusu sera ya EU na mahitaji ya Waukraine na wakimbizi wengine, Tume ya Ulaya ilisema katika barua pepe Jumanne kuwa itafanya “haraka kupendekeza (ili) kutumika kwa Kanuni ya Muda ya Kuwalinda ili kutoa msaada wa haraka na wenye ufanisi kwa watu wanaokimbia vita huko Ukraine.

Tume hiyo iko tayari kuzisaidia nchi wanachama kutoa hifadhi salama kwa watu wanaokimbia kutoka Ukraine na inafanya kazi kuandaa mpango wa jumla wa dharura wa kukabiliana na uchokozi wa Russia, ikijumuisha ulinzi wa watu wa Ukraine. …Tuna fikiria hatua zote zinazoweza kuchukuliwa kuyasaidia mataifa wanachama kuwashughulikia kwa haraka wanaowasili na kwa ufanisi. Mpaka tutakapo wasilisha mapendekezo yetu, hatuwezi kutoa maelezo zaidi.

Na kwa suala la watu wa rangi kuonewa, tume hiyo imesema: “Watu wote wenye shida, bila ya kujali utaifa wao, ukabila, au rangi ya ngozi zao, wanaokimbia vita iliyoko Ukraine wapewe ruhusa ya kuingia EU.

Waliochangia ripoti hii in pamoja na Mkuu wa Idhaa ya VOA Ulaya Mashariki Myroslava Gongadze, Grace Alheri Abdu wa Idhaa ya Hausa, Ignatius Annor wa idhaa ya Kiingereza kwa Afrika, na Betty Ayoub na Carol Guensburg wa Kitengo cha Africa