Matamshi ya Morrison wakati akizungumza na wanahabari yanatofautiana na yale yaliyotolewa na serikali yake wiki iliyopita, kwamba ingetoa msaada wa kiufundi pekee kwa taifa hilo. Sasa Morrison amesema kwamba taifa lake litanunua silaha kwa ajili ya Ukraine ikiwa sehemu ya juhudi za pamoja za mataifa mengine ya magharibi za kusaidia taifa hilo kujilinda dhidi ya uvamizi uliyofanywa na Russia.
Hata hivyo haijabainika ni lini silaha hizo zitapelekwa. Kando na ahadi hiyo, serikali ya Australia inasema itachangia dola milioni 25 zikiwa msaada wa kibinadamu kwa mashirika ya kimataifa yanayosaidia watu waliokwama Ukraine. Maelfu ya watu tayari wametoroka nchini humo na kuingia kwenye mataifa jirani, tangu kutokea uvamizi huo. Morrison hata hivyo ameongeza kwamba Australia haitotuma wanajeshi wake kusaidia moja moja kwenye vita hivyo.