Maafisa wa Ukraine wamewataka washirika wao wa Magharibi kuwapatia ndege za kivita ili kujibu kwa nguvu uvamizi wa Russia, lakini hadi sasa wito huo umepokelewa kwa tahadhari.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kama Ufaransa huenda inafikiria kuipa Ukraine ndege za kivita, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema Jumatatu kuwa “hakuna kilichowekwa pembeni” lakini alielezea masharti kadhaa kabla ya hatua kama hiyo kuchukuliwa.
Hiyo inajumuisha kuwa vifaa hivyo vya kijeshi havitagusa ardhi ya Russia, havitasababisha kusambaa zaidi kwa mivutano na “kutodhoofisha uwezo wa jeshi la Ufaransa.”
Nchini Marekani, wakati Rais Joe Biden alipowasili White House Jumatatu, waandishi walimuuliza iwapo ataipatia Ukraine ndege za kivita aina ya F-16, Biden alijibu, “Hapana.”
Ukraine ilipata nguvu wiki iliyopita wakati Marekani na Ujerumani, kwa pamoja zilipoahidi kupeleka vifaru kwa Ukraine, baada ya Ujerumani kusita kwa wiki kadhaa kupeleka vifaru vyake vya kisasa aina ya Leopard 2 Ukraine.
Baadhi ya taarifa katika habari hii inatokana na mashirika ya habari ya AP, Reuters na AFP