Vyanzo hivyo vilisema kundi la wanamgambo wa CODECO, ambalo linadai kulinda maslahi ya watu wa kabila la Walendu, kwa mara nyingine lilishambulia watu kutoka kabila hasimu la Wahema.
Wapiganaji wa CODECO walifanya shambulio la kuvizia siku ya Jumamosi karibu na kijiji cha Tali ambapo waliwasimamisha watu 15 akiwemo mwanamke mmoja, alisema Jules Tsuba, kiongozi wa shirika la kiraia katika wilaya ya Djugu.
Wanamgambo hao waliwafunga Kamba na kuwavua nguo kabla ya kuwaua, baadhi ya waathirika “walikatwa koo, wengine waliuawa kwa risasi,” alisema.
Kulingana na chanzo kutoka mashirika ya kibinadamu, “miili ya waathirika ilikuwa na alama za kuteswa.”
Kiongozi wa wilaya ya Djugu Ruphin Mapela, alithibitisha vifo vya watu 15 katika shambulio hilo ambalo limetokea baada ya miezi kadhaa ya hali ya amani.
CODECO ni miongoni mwa makundi kadhaa yenye silaha yaliyosaini makubaliano ya amani mwaka uliopita baada ya mazungumzo yaliyofanyika mjini Nairobi.
Forum