Makundi mbali mbali ambayo ni pamoja na chama cha upinzani cha Peoples Democratic (PDP), makundi ya vijana na kundi la wafuasi wa chama tawala All Progressive Congress (APC) yamesema kuwa INEC imeshindwa kufikia kiwango kilicho tarajiwa cha kuendesha uchaguzi nchini Nigeria na hivyo imeshindwa kufuata miongozo yake ambayo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Mahmood Yakubu aliahidi na kukubali kuifuata katika mchakato wa uchaguzi.
Katika barua yake kwa maafisa wa INEC, Chama cha PDP kilisema kuwa mgombea wa chama chake Atiku Abubakar alisema kuna umuhimu kwa INEC iwe na utaratibu mzuri kutoa matokeo ya uchaguzi wa rais ya kila mgombea ambayo yalitoka kwenye vituo vya kupigia kura kwa ajili ya umma kuyaona.
Mapema wiki hii mgombea urais kutoka chama cha upinzani Atiku Abubakar aliongoza mamia ya wafuasi wake katika maandamano ya amani kupinga jinsi tume ya uchaguzi ilivyoshughulikia uchaguzi huo na kumtangaza mgombea wa chama tawala Bola Tinubu kuwa mshindi.
Atiku na viongozi wengine waaandamizi wa chama cha upinzani cha People's Democratic Party (PDP) waliwaongoza wafuasi waliokuwa wamebeba mabango yaliyosomeka: "Wanigeria wamepoteza imani na INEC", "Mwenyekiti wa INEC ajiuzulu", na " Matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2023 hayaonyeshi matakwa ya watu wa Nigeria".