Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Januari 24, 2025 Local time: 00:27

PDP waandamana kupinga matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais Nigeria


Wafuasi wa Peoples Democratic Party (PDP) waandamana katika makao makuu ya kitaifa ya Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (INEC) kupinga matokeo ya uchaguzi wa Februari 25 huko Abuja, Nigeria Machi 6, 2023. REUTERS
Wafuasi wa Peoples Democratic Party (PDP) waandamana katika makao makuu ya kitaifa ya Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (INEC) kupinga matokeo ya uchaguzi wa Februari 25 huko Abuja, Nigeria Machi 6, 2023. REUTERS

Wanachama wa chama cha upinzani cha People's Democratic Party nchini Nigeria waliandamana hadi ofisi za tume ya taifa ya uchaguzi Jumatatu kupinga matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais wa hivi karibuni.

Tume hiyo ilimtangaza mgombea wa chama tawala cha All Progressives Congress Bola Tinubu kuwa mshindi wa uchaguzi wa Februari 25, ambao ulikumbwa na matatizo ya kiufundi yaliyochelewesha upigaji kura. Vyama vya upinzani vinasema uchaguzi uliibiwa na kuibua changamoto za kisheria.

Mamia ya wafuasi wa chama cha upinzani cha People's Democratic Party waliimba walipokuwa wakiandamana hadi makao makuu ya taifa ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, au INEC.

Maandamano hayo yaliyoongozwa na mgombea urais Atiku Abubakar na maafisa wengine wa chama yaliandaliwa kupinga tangazo la wiki iliyopita la mgombea wa chama tawala Bola Ahmed Tinubu kama mshindi wa kura za urais za Februari 25.

Waandamanaji, wengi wao wakiwa na mavazi meusi, waliimba kwamba Abubakar alishinda kura na kusema INEC ni mlaghai aliyepindua matakwa ya watu.

"Tuna ushahidi kwamba tulishinda uchaguzi huu kwa kishindo, lakini tunachosema na tunachodai ni kwamba kwa sasa, Mahmood Yakubu hajafanya mapitio ya matatizo yaliopo anapaswa kupitia tena makosa hayo. Hayo ndiyo matakwa yetu" alisema Kola Ologbondiyan Msemaji wa kamati ya Kampeni ya urais ya PDP.

Paul Ibe, mshauri wa Abubakar kuhusu vyombo vya habari, pia aliandamana Jumatatu "Huu ni uchaguzi mbaya zaidi katika historia yetu ya kidemokrasia. Kulikuwa na matarajio mengi. Wananchi wa Nigeria walikuwa wanatafuta kiongozi ambaye atawaleta pamoja na kuanza mchakato wa uponyaji. Kile tulichonacho kwa kweli ni wizi" alisema Ibe.

Polisi waliokuwa na silaha nzito waliwazuia waandamanaji hao kuvamia majengo ya INEC. Maafisa wa INEC hawakuwahutubia wanachama wa chama walio na malalamiko.

Uchaguzi wa urais na ubunge ulikuwa na ucheleweshaji wa wafanyakazi na kushindwa kwa mfumo. INEC ilisema ucheleweshaji ulisababishwa na masuala ya vifaa na vitisho vya usalama katika baadhi ya maeneo.

Lakini mashine mpya za INEC za kuidhinisha wapiga kura zilishindwa kufanya kazi ipasavyo katika majimbo mengi.

Mwishoni mwa wiki, INEC ilifanya kikao na viongozi kukagua uchaguzi huo na kujiandaa vyema kwa uchaguzi wa ugavana Machi 11.

Wiki iliyopita, mgombea wa tatu Peter Obi alitangaza kuwa pia alishinda uchaguzi na atathibitisha hilo kwa Wanigeria mahakamani.

Siku ya Jumapili, balozi wa Marekani nchini Nigeria, Mary Beth Leonard, alisema uchaguzi wa rais umeshindwa kukidhi matarajio.

Tinubu ametoa wito wa kuwepo kwa umoja na kusema anataka pande zote kufanya kazi naye kwa ajili ya kuwa na nchi bora.

Wataalamu wanasema bila kujali jinsi mambo yatakavyokuwa, rais atakuwa na masuala makubwa ya kushughulikia, ikiwa ni pamoja na kuenea kwa ukosefu wa usalama, uchumi dhaifu, mifumo ya afya na elimu iliyo na matatizo.

XS
SM
MD
LG