Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Januari 03, 2025 Local time: 03:11

Wananchi Tanzania walalamikia tatizo la upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali


Makamu wa Rais wa Tanzania azindua mradi wa maji Kikafu - Bomang'ombe Mkoani
Makamu wa Rais wa Tanzania azindua mradi wa maji Kikafu - Bomang'ombe Mkoani

Wananchi nchini Tanzania wamelalamikia tatizo la  upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali, hali inayopelekea kutumia maji yasiyo safi na salama na kuwalazimu kina mama kutembea umbali mrefu kupata huduma hiyo.

Huku serikali ikieleza kuwa chanzo cha tatizo hilo ni ukuaji wa miji pamoja na matumizi kutoka chanzo kimoja kwa kipindi kirefu bila kufanyiwa mabadiliko.

Tatizo la upatikanaji maji limekuwa ni kilio cha wananchi wa Tanzania kwa muda mrefu sasa, na bado linaendelea kuathiri maisha ya wale wanaoishi pembezoni mwa miji. Hali hii imesababisha kina mama kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji.

Hamadi Mtoga, mkazi wa Tabora, amesema licha ya kuwepo kwa miundombinu ya maji katika maeneo mengi, bado upatikanaji wake umekuwa ni wa taabu kutokana na kukaa siku nyingi bila ya maji katika baadhi ya maeneo.

“Mfano, mkoani kwangu hapa maji kwa muda wa siku kumi na tano hayatoki. Sasa wananchi wa haya maeneo wanaishi vipi ? Tunarudi kule kuanza kufuata yale maji ambayo ni ya zama za zamani ambapo tulikuwa tumekwisha ziacha. Tunanza kusafisha visima tena ambavyo tunachangia na mifugo.”ameongezea Mtoga

Licha ya baadhi ya mikoa nchini Tanzania kuna vyanzo vikubwa vya maji kama vile Mkoa wa Mwanza ambao umepakana na Ziwa Victoria, wananchi wake bado wameendelea kulalamikia changamoto ya upatikanaji maji. Hali hii inawafanya wananchi kuona adha wanayopata kutokana na kutowajibika kwa serikali.

Ester Thomasi, ambae ni mwananchi na mkazi wa Mwanza, anasema serikali imekuwa ikitoa ahadi za mara kwa mara za kukamilisha miradi ya maji inayotekelezwa mkoani humo. Lakini ahadi hizo zimekuwa hazitekelezeki kwa wakati.

Thomasi amesema “tunasikia tu kwamba kuna miradi inakuja kufanywa, na unakuta serikali inatoa matamko mengi kwamba mradi mkubwa unakuja hapa na utasambaza maji. Hata hivyo, imekuwa ni ahadi ambayo haitekelezeki kwa wakati kama ambavyo wao wanasema.”

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Maji, Muhandisi. Maryprisca Mahundi, ameiambia Sauti ya Amerika kwamba upungufu wa maji unaendelea kutokea kutokana na ukuaji wa miji, ongezeko la shughuli za kiuchumi, pamoja na matumizi ya chanzo kimoja cha maji kwa muda mrefu.

Kauli mbiu ya Siku ya Maji Duniani 2024 ni 'Maji kwa Amani'. Naibu Waziri wa Maji, Muhandisi Mahundi, ameongeza kuwa upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa vijijini umefikia wastani wa asilimia 79.6, huku mjini ukiwa na wastani wa asilimia 90.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG