Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 02, 2025 Local time: 21:43

Vijana Tanzania waitaka serikali kuwekeza katika teknolojia ya 3D


Wanafunzi nchini Tanzania
Wanafunzi nchini Tanzania

Vijana nchini Tanzania wanaojishughulisha na utengenezaji wa maudhui na bidhaa mbalimbali kwa kutumia teknolojia ya 3D, wameitaka serikali kuwekeza katika teknolojia hiyo, ili kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Wameeleza kuwa teknolojia hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto kutokana na kukosekana kwa vifaa na elimu inayohitajika.

Teknolojia ya 3D imekuwa ikikua kwa kasi katika sehemu mbalimbali duniani, hasa katika nchi zilizoendelea. Imekuwa ikitumika katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa filamu na maonyesho ya sinema, tasnia ya uchapishaji, na ubunifu wa bidhaa mbalimbali.

Hizzer Haizer, mratibu wa sanaa za kidijitali kutoka Nafasi Art Dar es Salaam, amesema teknolojia ya 3D ni fursa ambayo vijana wa Kitanzania wanapaswa kujifunza kwa kuwa inaweza kuwapa ajira. Na kuitaka serikali kuwekeza katika tasnia hiyo ili kuwasaidia vijana wanaofanya kazi hizo kusonga mbele.

"Ni fursa zaidi kwa Watanzania na wasanii kujifunza mambo ya kiteknolojia na kuruhusu pia uwezekano wa kujiajiri kwani ni sekta inayokua kwa kasi. Natoa wito kwa serikali kuwekeza katika elimu ya teknolojia, hata kuanzia ngazi ya shule, ili kukuza vipaji vya watu tangu wakiwa wadogo, kwa kuwa kuna vipaji vingi sana vinavyoweza kutambuliwa na kustawishwa huko nje," alisema.

Haizer anaongeza kuwa changamoto zinazoathiri maendeleo ya teknolojia ya 3D nchini na kufikia idadi kubwa zaidi ya vijana ni pamoja na gharama kubwa na upatikanaji mdogo wa vifaa vinavyohitajika. Pia, kuna ukosefu wa elimu juu ya matumizi ya teknolojia hiyo, na hata wakati inapatikana, mara nyingi hutolewa kwa gharama kubwa.8

Devin Martine ni mkufunzi wa 3D aliyewahi kufanya kazi katika studio za WOTI DISNII Walt Disney huko Marekani. Kwa sasa, yupo Tanzania kwa lengo la kuelimisha vijana wa nchi hiyo jinsi ya kutumia teknolojia hii. Amesema kuwa kinachohitajika ni uwekezaji ili kufanikisha upatikanaji wa soko, kutokana na teknolojia hiyo kuwa mpya kwa Tanzania.

Alisema: "Kwa hiyo, kuhusu soko, lipo wazi. Kama nilivyosema, programu ni nafuu. Nafikiri hapa zaidi ni kuhusu uwekezaji ili kuanzisha biashara, kwani kwa sasa hazipo. Hata wengine huniambia kwamba kile ninachofanya hapa, ningeweza kufanya Marekani, lakini nafanya hapa kwa kuwa ni kitu kipya. Hata hivyo, ni suala la muda tu; katika kipindi cha miaka kumi ama ishirini ijayo, kutakuwa na kampuni nyingi zinazofanya kazi hapa."

Hata hivyo, Joseph Manjala, mmoja wa wanafunzi waliohudhuria mafunzo ya matumizi ya teknolojia ya 3D yanayotolewa na Nafasi Art jijini Dar es Salaam, anaeleza mojawapo ya matumizi ya teknolojia hiyo na kuwataka vijana wa Kitanzania kuitumia ipasavyo fursa hiyo.

Ukitaka kutengeneza filamu yenye mazingira ambayo si halisia, kama vile mtu akiwa anaogelea na kuna milima nyuma, ni fursa kubwa sana kwa vijana, hasa sisi Watanzania. Hii ni teknolojia mpya, hivyo ni lazima tuichangamkie, alisema Manjala.

Vijana hao wamemalizia kwa kuitaka serikali kuwekeza zaidi katika masuala ya teknolojia, kwani inaweza kusaidia kupunguza matatizo ya ajira kwa vijana wengi nchini.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika, Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG