Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Januari 24, 2025 Local time: 03:42

Waliofariki na kimbunga Freddy wazidi 240


Wanaume wakichimba kuwatafuta manusura na waathiriwa kwenye matope na vifusi vilivyosababishwa na Kimbunga Freddy huko Chilobwe, Blantyre, Malawi, Machi 13, 2023. Picha na Shirika la habari la REUTERS/Eldson Chagara.
Wanaume wakichimba kuwatafuta manusura na waathiriwa kwenye matope na vifusi vilivyosababishwa na Kimbunga Freddy huko Chilobwe, Blantyre, Malawi, Machi 13, 2023. Picha na Shirika la habari la REUTERS/Eldson Chagara.

Waokoaji walijitahidi siku ya Jumatano kuwafikia watu walionusurika na kimbunga Freddy kilichopiga mji wa Blantyre nchini Malawi.

Kimbunga hicho kimelikumba eneo hilo la kusini mwa Afrika kwa mara ya pili na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 240 katika nchi mbili - Malawi na Msumbiji.

Hali ya hewa ilitarajiwa kuwa shwari wakati dhoruba ikiondoka taratibu baada ya siku kadhaa za mvua kubwa, lakini radi zitaendelea kwenye maeneo hayo, wakati viwango vya mafuriko bado viko juu katika baadhi ya maeneo, na kuzuia juhudi za dharura.

"Idadi ya vifo imepanda kutoka 190 hadi kufikia 225 wakati watu 707 wamejeruhiwa na wengine 41 waliripotiwa kutojulikana walipo," idara ya kudhibiti majanga nchini Malawi ilisema.

Msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Malawi Felix Washon aliliambia shirika la habari la AFP kuwa wamekuwa wakiwaokoa watu waliokuwa kwenye miti na mapaa ya nyumba.

"Ni changamoto kuwafikia, maji ni mengi, na madaraja yamebomoka."

Freddy ilirejea kusini-mashariki mwa Afrika mwishoni mwa wiki kwa mara ya pili katika muda wa chini ya wiki tatu, na kusababisha vifo na uharibifu.

Mamlaka katika nchi jirani ya Msumbiji hadi sasa imeripoti vifo vya watu 21 -- na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.

Papa Francis aliwaombea waathirika wa kimbunga nchini Malawi, wakati wa mkutano wake wa kila wiki unaofanyika huko St Peter's Square.

"Ninawaombea waliofariki, waliojeruhiwa, waliokoseshwa makazi. Tunamuomba Mola azisaidie familia na jamii zilizoathirika zaidi na janga hili," alisema.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP.

XS
SM
MD
LG