Kimbunga Freddy, kinachoelekea kuwa dhoruba ya muda mrefu iliyovunja rekodi ya kudumu, kilipiga sehemu za kusini mwa Afrika mwisho mwa wiki kwa mara ya pili ndani ya wiki chache, na kurejea tena baada ya mara kwanza kupiga katika eneo hilo mwishoni mwa mwezi.
Zaidi ya miili ya 60 ilipatikana wakati wa mchana katika eneo la kusini mwa Malawi ambako mvua kubwa ilisababisha mafuriko, kwa mujibu wa taarifa kutoka shirika la Msalaba Mwekundu.
"Watu 66 wamefariki nchini Malawi, 93 wamejeruhiwa na watu 16 hawajulikani walipo kutokana na Kimbunga cha Tropiki cha Freddy," shirika la misaada ya kibinadamu, ambalo linasaidia katika shughuli za uokoaji na utafutaji, liliandika kwenye Twitter.
Rais wa nchi hiyo Lazarus Chakwera alitangaza "hali ya hatari katika eneo la Kusini" mwa nchi nchi hiyo baada ya "kuelezea wasiwasi mkubwa kuhusu uharibifu uliosababishwa na kimbunga Freddy ".
Malawi ni moja ya nchi maskini sana duniani, tayari imeanza kuomba misaada kwa familia zilizoathirika kutoka mashirika ya misaada ya ndani na ya kimataifa, ilisema.
Takriban miili ya watu 36 ilipatikana katika kitongoji kimoja cha Chilobwe, mjini Blantyre, jiji kubwa lenye zaidi ya watu milioni moja, msemaji wa polisi wa eneo hilo Beatrice Mikuwa alisema, na kuongeza kuwa mji huo "uliathirika zaidi", huku dazeni ya nyumba zikiwa zimesombwa na maji.
Malawi imeamuru shule katika wilaya kumi za kusini kuendelea kufungwa hadi Jumatano, huku mvua na upepo ukitarajiwa kuendelea kulikumba eneo la kusini mwa taifa hilo.
Shirika la ndege la Malawi lilisema safari zote za ndege kwenda Blantyre zimefutwa mpaka itakapo tangazwa tena. Hatua hii inafuatia ndege iliyokuwa ikielekea katika uwanja wa ndege wa Blantyre kukumbana na hali mbaya ya hewa katikati ya safari na kulazimika kurudi katika mji mkuu Lilongwe.
Idadi ya vifo ilitarajiwa kuongezeka, wakati mamlaka zilifanya jitihada za kuyafikia maeneo yote yaliyoathiriwa.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Agence France-Presse