Hii ni moja ya dhoruba kali zaidi kuwahi kurekodiwa katika ukanda wa kusini wa dunia, Freddy kinaweza pia kuvunja rekodi ya kimbunga cha tropiki kilichodumu kwa muda mrefu zaidi, kulingana na taarifa ya Shirika la hali ya hewa duniani, ambalo lilisema rekodi iliyopo inaonyesha kimbunga kilichodumu kwa muda mrefu zaidi kilikuwa mwaka 1994 ambacho kilidumu kwa siku 3.
Kimbunga cha Freddy kilitangazwa kwa mara ya kwanza tarehe 6, mwezi Februari, ambazo ni siku 33 zilizopita.
Zaidi ya watu 171,000 waliathirika kutokana na kimbunga hicho kilipopita katika eneo la kusini mwa Msumbiji wiki mbili zilizopita, na kusababisha mvua kubwa na mafuriko ambayo yaliharibu nyumba na mazao, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu la OCHA.
Siku ya Ijumaa OCHA ilitoa idadi mpya ya vifo vilivyosababishwa na kimbunga Freddy kufikia watu 27,10 nchini Msumbiji na watu 17 huko Magascar.
Kulingana na shirika la kitaifa la kudhibiti majanga Msumbiji, takriban watu 565,000 nchini huenda wako hatarini kuathiriwa na kimbunga hicho ambacho kinatarajiwa kuyakumba majimbo ya Zambezia, Tete, Sofala na Nampula wakati jimbo la Zambezia likitarajiwa kuathirika zaidi.
Msemaji wa Shirika la hali ya hewa duniani Clare Nullis aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa dhoruba hiyo inatarajiwa kusababisha mvua kubwa sana katika sehemu za Msumbiji pamoja na maeneo ya kaskazini mashariki mwa Zimbabwe, kusini mashariki mwa Zambia na Malawi.
Duniani kote, mabadiliko ya hali ya hewa yamekuwa yakisababisha vimbunga vinavyoambatana na dhoruba zenye mvua kubwa na upepo mkali, wanasayansi wanasema. Bahari hunyonya kiasi kikubwa cha joto kinachotokana na gesi chafu, na wakati maji ya bahari yenye uvuguvugu yanapopeleka angani nishati yake ya joto na kuchochea dhoruba.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters