Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 15:59

Wagombea urais Marekani wafanya mikutano ya mwisho mwisho kabla ya uchaguzi


Mgombea urais wa chama cha Demokratik Kamala Harris (kulia) na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump. Picha na AFP
Mgombea urais wa chama cha Demokratik Kamala Harris (kulia) na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump. Picha na AFP

Wagombea urais nchini Marekani, Kamala Harris na Donald Trump, wanaendelea na harakati za mwisho mwisho, kuelekea kwa uchaguzi wa Jumanne wiki ijayo, ambao unaelezwa kama wenye ushindani mkali zaidi.

Wawili hao wanahutubia mikutano ya kampeni katika majimbo mbalimbali, hasa yale ambayo utafiti unaonyesha, ndiyo yatakayoamua mshindi wa kinyang’anyiro hicho.

Ikiwa ni wikendi ya mwisho kabla ya uchaguzi wa urais wa Marekani wa Novemba 5, wagombea wote wamekita kambi katika majimbo muhimu, kuwarai wapiga kura kujitokeza na kwa wingi, wakifanya mikutano katika majimbo kama vile Michigan, Wisconsin, North Carolina.

Jumamosi wawili hao wanafanya mikutano katika jimbo la North Carolina, ikiwa ni mara ya nne kwao kufanya mikutano ya kampeni katika jimbo moja kwa siku moja, hii ikiashiria jinsi baadhi ya majimbo yanavyopewa umuhimu na viongozi hao, kwelekea uchaguzi wa Jumanne.

Harris kayika mikutano yake ya kampeni kwenye jimbo la Michigan, na kwingineko, ambako amkuwa mara kwa mara akiandamana na baadhi ya nyota wenye ushawishi, amekuwa akisisitiza umuhimu wa umoja na demokrasia. Harris pia alitarajiwa kutembelea majimbo mengine, akisisitiza dhamira yake ya kulinda haki za uzazi na kushughulikia mabadiliko ya tabianchi.

Katika makutano na ushirika wa wa wafanyikazi wa jimbo la Wisconsin, Harris aliahidi kuwekeza katika viwanda, na pia kufungua fursa mpya za utengenezaji wa vifaa muhimu vinavyozingatia usafi wa mazingira. Alimkosos mpinzani wake, Donald Trump, akisema kwamba hajali maslahi ya wafanyakazi

"Kwa sababu anazungumza sana. Lakini ukitazama kwa makini, kile ambacho amekifanya, ukIangalia kwa makini ni nani aliyemsaidia, wakati watu walihitaji mlinzi na rafiki, utaona kwa kweli ni mtu wa aina gani. Na ni lazima tusambaze ujumbe, kuelezea yeye ni mtu wa aina gani, kwa sababu kuna taarifa potofu sana huko nje, kuhusu yeye ni nani, na ni nini anakisimamia," alisema.

Harris amewaambia wafuasi wake katika mikutano kadhaa wiki hii kwamba, iwapo atachaguliwa, atajikita katika kutekeleza ahadi zake za kampeni, na kwamba mpinzani wake atazingatia kulipiza kisasi. Lakini Trump anasema, yeye ndiye mwenye rekodi ya kuibadilisha Marekani, na kwamba Harris hawezi kuiongoza nchi, kwa sababu, akiwa makamu wa rais wa sasa Joe Biden, tayari ameivuruga.

"Kamala ambaye hana uwezo kabisa aliivuruga, nitairekebisha, tutairekebisha, tutairekebisha haraka, Amerika itakuwa kuu, bora, shupavu, tajiri, salama na yenye nguvu kuliko hapo awali," alisema.

Ukusanyaji wa maoni unaonyesha kinyang’anyiro kikali, bila tofauti kubwa kati ya wagombea hao wawili, kwenye majimbo muhimu.

Lakini je, Wamarekani wanategemea kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa maoni? Dkt Timothy Sadera ni mchambuzi wa siasa za Marekani.

Anasema mara nyingi ukusanyaji wa maoni hauonyeshi picha halisi ya mambo.

"Inategemea pia ni nani aliyejibu maswali na ni maswali yapi yaliyoulizwa," amesema.

Zaidi ya kura milioni 60 tayari zimepigwa kupitia upigaji kura wa mapema.

Kati ya masuala muhimu ambayo wapiga kura wengi wanaangazia mwaka huu ni Uchumi, uhamiaji, afya, mabadiliko ya hali ya hewa na usalama wa taifa.

Lakini siyo kinyanga’anyiro cha urais ambazcho kinavutia hisia. Yeyote atakayechaguliwa kama rais, kwa kiasi kikubwa atahitaji uungwaji mkono katika baraza la wawakilishi na lile la seneti, ili kutekeleza sera na ajenda zake kikamilifu.

Hatua za mwisho za kujaribu kuwashawishi wapiga kura ambao bado hawajaamua ni nani wa kumuunga mkono, zinaweza kuwa na athari kubwa kwa mustakabali wa siasa za Marekani.

Forum

XS
SM
MD
LG