Sudan inatumbukia kwenye lindi la maafa na uharibifu kwa kasi kubwa, mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, alionya alipokuwa akiwataka wafadhili kuingilia kati na kuzuia ongezeko la vifo kutokana na vita hivyo.
Mkutano huo ulifanyika katikati ya usitishaji mapigano wa siku tatu, ambao ulionekana kuleta utulivu katika mji mkuu Khartoum, baada ya kushindwa kwa mapatano ya awali, ya wezesha misaada kufikia wanaoihitaji.
"Leo, wafadhili wametangaza karibu dola bilioni 1.5 kwa ajili ya kuitikia wito wa kibinadamu kwa Sudan na eneo hilo," mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Martin Griffiths alisema, akifunga mkutano ulioandaliwa mjini Geneva, Uswizi.
"Mgogoro huu utahitaji usaidizi endelevu wa kifedha na ninatumai sote tunaweza kuiweka Sudan katika nafasi ya kwanza ya vipaumbele vyetu."
Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuwashughulikia wakimbizi Filippo Grandi aliongeza kwamba "Ni muhimu sana michango hiyo kugawanywa kwa uwazi na kutolewa haraka iwezekanavyo kwa sababu kuna uhaba wa fedha."
Zaidi ya miezi miwili baada ya mapigano, Umoja wa Mataifa una wasiwasi kwamba mgogoro huo unaweza kusambaa na kuyumbisha mataifa jirani ya Afrika.
"Kiwango na kasi ambayo Sudan inashuka kwelekea hali ya maafa na uharibifu haijawahi kutokea," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Guterres aliuambia mkutano huo.
Forum