Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 08:07

Tanzania: Wanafunzi wa udaktari wa Sudan wapatao 150 wapokelewa Hospitali ya Taifa ya Muhimili kuendelea na masomo


Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Khartoum.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Khartoum.

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili nchini Tanzania imepokea wanafunzi wa udaktari wapatao 150 kutoka katika chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia Khartoum nchini Sudan.

Wanafunzi hao walikimbia machafuko yanayoendelea nchini mwao kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe huku uongozi wa hospitali hiyo umewapatia hifadhi mpaka pale machafuko yatakapokwisha.

Mapigano ambayo yanaendelea nchini Sudan yanaendelea kusababisha maafa kwa maelfu ya raia wa taifa hilo kuikimbia nchi yao huku wanafunzi wakiwa ni miongoni mwa waathirika wa machafuko hayo.

Hali hiyo imepelekea wanafunzi wa udaktari 150 kuomba kuendelea na masomo yao ya mwaka wa mwisho katika hospitali ya taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Profesa Mamoun Homeida ambaye ni makamu mkuu wa chuo kikuu cha sayansi na teknolojia Khartoum amesema wanaushukuru uongozi wa muhimbili kwa mapokezi mazuri waliyoyapata na wameichagua Tanzania kati ya nchi za Afrika kwasababu ya amani iliyopo nchini humo pamoja na uwezo mkubwa wa kitaaluma ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika.

“Tuna mahusiano mengi na nchi nyingi za Kiafrika, Tanzania imechaguliwa kwa sababu ni nchi imara na ina amani na jina la Dar es Salaam lina maana ni nyumba ya amani na hilo ni namba moja katika usalama. Kitaaluma fani ya udaktari ni kubwa sana miongoni mwa nchi za Afrika’’

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Khartoum Sudan
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Khartoum Sudan

Tanzania na Sudan zimekuwa na uhusiano wa karibu kwa miongo mingi ambao umelifanya taifa hilo kuwa kimbilio lao la kwanza. Hata hivyo Profesa Mohammed Janabi ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa hospitali ya taifa ya Muhimbili amewahakikishia kuwa wamekuja sehemu sahihi na watafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanafunzi hao wanamaliza masomo yao kwa salama na amani.

Profesa Janabi anaeleza: Wamekuja sehemu sahihi ambayo sisi wote hapa tuliopo muhimbili timu ya usimamizi walimu madaktari wauguzi tutafanya linalowezekana sisi hatuna pingamizi hata kama hali itatulia karibuni kama wataridhia kuendelea kukaa mpaka pale watakapomaliza mwaka wa tano hio ni sawa kwamba itafika muda wamemaliza chuo hawana mahali pakwenda kufanya mafunzo kazini sisi tutakuwa tayari kabisa kuwapokea.

Hata hivyo kwa upande wa wanafunzi hao ambao wameonyesha kuwa na nyuso zilizojawa na furaha wameiambia sauti ya Amerika kuwa wamefurahishwa na ukarimu wa Watanzania. Rubaa Anwar ambaye ni kiongozi wa wanafunzi hao anaelezea zaidi:

“Tumefurahishwa na mapokezi tuliyoyapata, ni juu ya matarajio yetu na kama profesa Mahmoun alivyokwisha eleza tumesafiri kutoka mbali sana kupata maarifa yote ambayo tunaweza kupata tumebahatika kupatiwa hifadhi tayari tumeshasoma na kiasi cha maarifa ambacho tumepata kwa wiki moja tu ni zaidi ya matarajio yetu.’’

Daktari Janabi amewataka madaktari wenzake kuwapa ushirikiano wanafunzi hao kwa kipindi chote watakachokuwa hapa nchini kwani wapo katika kipindi kigumu ambacho kinahitaji faraja zaidi.

Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG