Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 21:16

Wadhibiti Marekani wathibitisha kidonge cha majaribio cha COVID-19 kinatibu


Kampuni ya madawa ya Merck & Co. ikionyesha dawa yake mpya ya kutibu COVID-19 (Merck & Co. via AP, File)
Kampuni ya madawa ya Merck & Co. ikionyesha dawa yake mpya ya kutibu COVID-19 (Merck & Co. via AP, File)

Wadhibiti wa Afya wa Serikali Kuu ya Marekani wanasema kidonge cha majaribio cha kutibu COVID-19 kutoka kampuni ya kutengeneza dawa ya Merck kinatibu virusi.

Hata hivyo FDA imeeleza wataomba mawazo kutoka kwa wataalam wa nje juu ya hatari za matatizo ya wakati wa kujifungua na matatizo mengine yanayoweza kutokea wakati wa ujauzito.

Idara ya Kusimamia Ubora wa Chakula na Dawa, FDA, imetoa uchambuzi wake juu ya dawa hiyo kabla ya mkutano wa umma wiki ijayo ambapo wanazuoni na wataalam wengine watatoa mawazo yao juu ya usalama na uwezo wa tiba hiyo. Idara hiyo hailazimiki kufuata ushauri wa kikundi hicho.

Wanasayansi wa FDA wamesema tathmini yao imetambua uwezekano wa kuwepo hatari kadhaa, ikiwemo madhara kwa kiumbe kinachokua wakati wa ujauzito na matatizo ya kujifungua yaliyotambuliwa katika utafiti wa dawa hiyo kwa Wanyama.

Kutokana na hatari hizo FDA itawauliza washauri wake Jumanne ijayo iwapo dawa hiyo isitolewe kabisa wakati wa ujauzito au inaweza kutolewa katika baadhi ya hali za wagonjwa wajawazito.

Kutokana na hali hiyo, FDA imesema dawa hiyo itakuwa na tahadhari juu ya hatari za kutumia wakati wa ujauzito, lakini madaktari bado watakuwa na fursa ya kuitoa kwa baadhi ya wagonjwa iwapo faida zake zitakuwa zaidi ya hatari zake kwa wagonjwa.

Kutokana na wasiwasi wa usalama wake, FDA imesema Merck wamekubali kuwa dawa hiyo isitolewe kwa watoto.

Athari nyingine za dawa hiyo zilionyesha kuwa hafifu na nadra kutokea, ambapo asilimia 2 ya wagonjwa walishikwa na tumbo la kuendesha.

Wasimamizi pia wameeleza kuwa Merck ilikusanya takwimu kidogo zaidi za usalama wa dawa yake hiyo kwa jumla ukilinganisha na zile zilizokusanywa kwa matibabu mengine ya COVID-19.

FDA itawataka washauri wa kujitegemea kujadili masuala yote hayo na halafu wapige kura iwapo faida ya dawa hii inapita madhara yake.

XS
SM
MD
LG