Hatua hiyo ilijadiliwa na maseneta wa vyama vya Demokratic na Republican wakati wa mazungumzo ya miezi kadhaa na inaungwa mkono na Rais mdemokrat, Joe Biden.
Lakini Spika wa baraza la wawakilishi Mike Johnson, ambaye ndiye kiongozi wa walio wengi wa chama cha Republican, mara moja alitangaza kwamba mswaada huo "hautapitishwa," kwenye baraza la wawakilishi, akisema hauna nguvu ya kutosha ya kudhibiti ipasavyo, uhamiaji kwenye mipaka ya Marekani.
Kiongozi wa Walio Wengi katika Seneti Chuck Schumer alipanga kura ya awali juu ya hatua hiyo, ipigwe Jumatano wiki hii, akisema vipaumbele vya mswaada huo "ni muhimu sana na havifai kupuuzwa, wala kuruhusu siasa kuingilia kati.
Aliita sheria hiyo "hatua kuu kuelekea kuimarisha usalama wa kitaifa wa Marekani, nje ya nchi na kando ya mipaka yetu," ambako maelfu huvuka kila siku kutoka Mexico na kuingia Marekani.
Mswaada huo unaahidi dola bilioni 60 za msaada mpya kwa Ukraine ili kuendeleza vita vyake vya karibu miaka miwili dhidi ya uvamizi wa Russia, wakati Israeli itapata msaada wa kiusalama wa dola bilioni 14, huku dola bilioni 10 zikienda kwa misaada ya kibinadamu kwa raia katika maeneo yenye migogoro kama vile Ukraine, Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel.
Dola nyingine bilioni 2.4 zingefadhili juhudi za kijeshi za Marekani kukabiliana na mashambulizi katika Bahari ya Sham, huku dola bilioni 4.8 zikiwasaidia washirika wanaokabiliana na uvamizi wa Wachina katika eneo la Indo-Pasifiki.
Forum