Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 20:57

Waandamanaji nchini Nigeria wakabiliwa na adhabu ya kifo


Waandamanaji wakiwa mahabusu baada ya kesi kusikilizwa mahakamani huko Abuja Septemba 2, 2024. Picha na AP/Olamikan Gbemiga
Waandamanaji wakiwa mahabusu baada ya kesi kusikilizwa mahakamani huko Abuja Septemba 2, 2024. Picha na AP/Olamikan Gbemiga

Waandamanaji wasiopungua 10 nchini Nigeria wanakabiliwa na adhabu ya kifo Jumatatu baada ya kushtakiwa kwa uhaini kutokana na kushiriki kwao katika maandamano ya hivi karibuni katika moja ya migogoro mibaya zaidi kiuchumi nchini humo.

Waandamanaji hao walifikishwa mahakamani katika mji mkuu, Abuja, na kushtakiwa kwa "nia ya kuleta machafuko nchini Nigeria... na kumtisha rais" wakati wa maandamano hayo. Walikana mashtaka na wameendelea kushikiliwa gerezani hadi kusikilizwa kwa ombi la dhamana Septemba 11.

Raia mmoja wa Uingereza alitajwa miongoni mwa washukiwa ambao bado hawajakamatwa. Ubalozi wa Uingereza haukujibu ombi la kutoa maoni mara moja.

Msemaji wa polisi wa Nigeria, Muyiwa Adejobi, alimshutumu Andrew Wynne kwa kufanya kazi na waandamanaji kama mamluki wa kigeni na kuunda "mtandao wa vikundi vya siri ili kuipindua serikali na kuingiza taifa katika machafuko." Hakutoa ushahidi wowote kuunga mkono madai hayo.

Amnesty International imesema kuwa waandamanaji wasiopungua 22 walipigwa risasi na kuuawa na vikosi vya usalama wakati wa maandamano hayo. Mamlaka zimekanusha madai hayo. Associated Press ilithibitisha mauaji ya watu watatu.

Mpaka sasa hatima ya mamia ya waandamanaji wengine waliokamatwa haijulikani.

Kumekuwa na wasiwasi unaoongezeka nchini Nigeria kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu chini ya serikali ya Rais Bola Tinubu, ambaye alichaguliwa mwaka jana baada ya kuahidi mabadiliko chanya.

Waandamanaji walishtakiwa chini ya Sheria ya Adhabu ya Nigeria, ambayo wakosoaji wameielezea kama moja ya sheria kali zaidi nchini humo na inayotumiwa na mamlaka kuzima upinzani. Shtaka la uhaini lina adhabu ya kifo.

“Baadhi ya mashtaka yanaonyesha jinsi mamlaka ya Nigeria yanavyoweza kwenda mbali katika kutumia vibaya mfumo wa haki ya jinai ili kunyamazisha sauti za wakosoaji. Haya ni mashtaka yaliyotungwa wazi ambayo lazima yafutwe mara moja,” Mkurugenzi wa Amnesty nchini, Isa Sanusi, alisema katika taarifa.

Forum

XS
SM
MD
LG