Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 06:20

Vurugu za Afrika zinakiuka mafundisho ya Yesu


Mwanamume anayemwigiza Yesu Kristo msalabani siku ya Ijumaa Kuu mjini Lagos, tarehe 14 Aprili 2017. Picha na PIUS UTOMI EKPEI / AFP.
Mwanamume anayemwigiza Yesu Kristo msalabani siku ya Ijumaa Kuu mjini Lagos, tarehe 14 Aprili 2017. Picha na PIUS UTOMI EKPEI / AFP.

Wakristo wa madhehebu mbali mbali ya Afrika Mashariki, wametoa wito kwa waumini duniani kutafakari na mateso, kifo pamoja ufufuo wa Yesu ili kuleta amani na utulivu katika bara la Afrika.

Wakizungumza na Sauti ya Amerika kwa njia ya simu, katika kipindi hiki ambacho wakristo duniani kote wanajiandaa kusheherekea sikukuu ya Pasaka wamesema ubinafsi, dhuluma, mapigano yanayoendelea katika maeneo mbalimabli ya bara la Afrika yanakwenda kinyume na ujumbe pamoja na mafundisho ya Yesu na kusababisha mateso na umaskini kwa jamii.

Padri wa kanisa la katoliki dayosisi ya Bukavu katika jimbo la Kivu Kusini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo profesa Jean- Bosco Bahala, amesema wakati wakristo duniani wakisherehekea ufufuo wa Yesu Kristo siku ya Pasaka na Ijumaa Kuu wanapaswa kukumbuka mafundisho yake yakiwemo ya ujumuishaji wa watu wote.

“Yesu aliwaokoa watu wote, wazuri na wabaya na pembeni yake walikuwepo wahalifu wawili, na aliwaambia kuwa watakuwa naye akiwa paradiso” amesema padri Bahala.

Amewaasa waumini wa dini ya kikristo kushikamana na waache vitendo vya ubinasfi, ukatili na dhuluma ambavyo ndiyo chanzo cha vurugu na mateso huko DRC, Nigeria na maeneo mengine barani Afrika.

Maria Salome Augustino mkazi wa jiji la Mwanza Tanzania, amesema “kifo cha Yesu na Ufufuo wake utakuwa na maana zaidi endapo amani na utulivu utaimarishwa katika jamii”

Waumini wa kanisa la Katoliki huko Kibera, Nairobi siku ya Ijumaa kuu tarehe 7 Aprili, 2023. Picha na Yasuyoshi CHIBA / AFP.
Waumini wa kanisa la Katoliki huko Kibera, Nairobi siku ya Ijumaa kuu tarehe 7 Aprili, 2023. Picha na Yasuyoshi CHIBA / AFP.

Akisisitiza uwepo wa upendo na amani Zidonia Makoba mkazi wa Dar Es Salaam ametoa ujumbe wake kwa kusema “ Kristo afufuke ndani yako”.

Katika ujumbe wa Ijumaa takatifu na pasaka, naye mhadhiri mwandamizi wa Chuo kikuu cha kikristo cha Uganda kilichopo, Mukono, nje ya mji wa Kampala, amesema pamoja na kwamba Yesu alikufa msalabani kwa ajili ya ubinadamu, lakini hivi sasa jamii nyingi zinakiuka maadili yake ambapo mifumo ya haki imetawaliwa na watu wenye mabavu.

Wakristo duniani kote wanajiandaa kusherehekea sikukuu ya Pasaka siku ya Jumapili.

Wiki kabla ya Pasaka inajulikana kama Wiki Takatifu, ambayo huanza baada ya kumalizika kwa siku 40 za Kwaresima. Ijumaa Kuu hufanyika siku mbili kabla ya Pasaka.

Ijumaa kuu ni siku ambayo makanisa ya Kikristo na ya Kikatoliki huadhimisha kusulubiwa na kifo cha Yesu Kristo. Ijumaa Kuu ni sehemu muhimu katika historia ya misingi ya kikristo kwa sherehe za Pasaka.

-Imetayarishwa na Mariam Mniga, VOA, Washington DC.

XS
SM
MD
LG