Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 22:09

Maandamano hayata muondoa Ruto madarakani


Rais wa Kenya William Ruto akiongea na makatibu wake wapya wa baraza la mawaziri Ikulu ya Nairobi Oktoba 27, 2022. Picha na Simon MAINA / AFP.
Rais wa Kenya William Ruto akiongea na makatibu wake wapya wa baraza la mawaziri Ikulu ya Nairobi Oktoba 27, 2022. Picha na Simon MAINA / AFP.

Maandamano yaliyoitishwa na mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ya kuupinga utawala wa rais William Ruto hayataweza kumuondoa madarakani rais huyo mbali na kuwepo kwa changamoto za kiuchumi zinazoikabili Kenya.

Kuilingana na tathmini iliyotolewa na baadhi ya wataalam wa masuala ya amani, migogoro ya kisiasa na harakati za kijamii katika vyuo vikuu nchini Marekani na Kenya wamesema ni vigumu kumuondoa madarakani kiongozi ambaye alichaguliwa katika misingi ya kidemokrasia.

Stephen Zunes ambaye ni profesa katika Chuo Kikuu cha San Francisco kilichopo katika jimbo la California aliiambia Sauti ya Amerika kuwa kiongozi huyo alichaguliwa na watu katika misingi ya kidemokrasia, mbali na kuwa rushwa ni tatizo lakini mfumo uliopo si wa utawala wa mtu mmoja, kwa hiyo ni vigumu sana maadamano kumuondoa madarakani ”

Naye profesa Ken Opalo kutoka Walsh School of Foreign Service iliyoko katika chuo kikuu cha Georgetown, kilichopo katika jiji la Washingiton DC, amesema maandamano hayo hayana nguvu ya kutosha kuiondoa serikali iliyochaguliwa kihalali madarakani “Wakenya wengi wanaona utawala wa sasa umeingia madarakani kihalali na kwa hivyo ni halali.”

Maandamano hayo ambayo yamekuwa yakifanyika kwa wiki ya pili yamesababisha vifo vya watu wawili, huku uporaji na ghasia zikiongezeka wakati polisi wakitumia mabomu ya kutoa machozi na maji yanayowasha wakipambana na waandamanaji katika maeneo ya Nairobi pamoja na Kisumu.

“Mimi nadhani, maandamano haya hayatadumu, yatakwisha hivi karibuni, hayatasababisha mabadiliko ya serikali au kitu chochote, lakini yanatuma ujumbe kuwa watu wamechoshwa sana” Alisema Zunes.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga (katikati) akizungumza na wafuasi huko Nairobi mnamo Machi 20, 2023. Picha na YASUYOSHI CHIBA/AFP.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga (katikati) akizungumza na wafuasi huko Nairobi mnamo Machi 20, 2023. Picha na YASUYOSHI CHIBA/AFP.

Mhadhiri wa chuo kikuu cha Ufundi cha Mombasa katika idara ya sayansi ya jamii, Wilson Ndenyele amesema vurugu zilizotawala nchini humo zinatokana na mabadiliko ya utawala kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.

Wataalamu hao wamesema wananchi wa Kenya wana hasira ya kupanda kwa gharama za maisha na serikali kushindwa kushughulikiaa tatizo hilo kama alivyoahidi Rais Ruto wakati wa kampeni kuwa ataboresha maisha ya wakenya ikiwemo ongezeko la ajira kwa vijana na kushuka kwa bei za bidhaa na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wadogo.

“Rais William Ruto aliahidi kutimiza mengi katika siku zake 100 za kwanzo madarakani, na bado hajatimiza.” Alisema profesa Opalo.

Hata hivyo wamesema maandamano hayo yasidharauliwe na ni mapema kutabiri kitakachotokea na kwamba inategemea jinsi gani serikali ya Ruto itakavyokabiliana na maadamano hayo ambayo yanatakiwa kufanyika mara mbili kwa wiki.

Wakati huo huo Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa rais Ruto ambaye yuko katika ziara nchini Ujerumani Jumanne alionya kuwa atawashughulikia wale wote waliohusika katika uhalifu wakati wa maandamano yaliyofanyika Jumatatu,

Umoja wa nchi za Afrika siku ya Jumanne ulitoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kisiasa na utulivu, kufuatia maandamano ya kuipinga serikali nchini humo.

Mkuu wa Tume ya AU Moussa Faki Mahamat alielezea "wasiwasi mkubwa" kuhusiana na ghasia hizo na kuomba utulivu.

-Imetayarishwa na Mariam Mniga, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG