Katika mkutano huo unaofanyika jijini Dar es Salaam kujadili rasilimali watu barani Afrika ili kumuuinua kijana, wasomi hao wamesema, ni kawaida kwa viongozi wa nchi kukubaliana juu ya masuala mbalimbali kwenye mikutano, lakini utekelezaji wake wa vitendo ndio unaohitajika katika kuleta matokeo chanya.
Mhadhiri msaidizi chuo kikuu cha Dodoma katika idara ya sayansi ya siasa na utawala wa umma, Edson Mhowera amesema yote yaliyo jadiliwa yatengenezewe mfumo ambao utasaidia kupelekea kwenye utekelezaji.
“Yaende kwenye utekelezaji yatengenezewe mfumo ambao wakuweza kufanyiwa tathimini kwamba je mwaka 2023 tulikutana Dar es Salaam tuliazimia moja mbili tatu baada ya muda fulani je katika yale tuliyo yaazimia kwa kiwango gani tumeweza kutekeleza ili isiwe kama ni kusanyiko ambalo halina manufaa lazima liwekewe malengo ili kuweza kutoka hapa tulipo”, alisema Mhowera.
Kwa sasa Afrika ndio bara litakalokuwa na vijana wengi zaidi ifikapo mwaka 2030, ambapo idadi ya vijana wakati huo itakuwa asilimia 42 ya vijana wote duniani. Kwa hiyo uwepo wa asilimia kubwa ya vijana katika bara la Afrika kunaweza kuwa na tija iwapo viongozi wa Afrika watawekeza katika rasilimali watu kwa kuhakikisha uwepo wa afya na elimu bora yenye stadi za maisha ili kujenga nguvu kazi yenye tija.
Msimamizi katika idara ya Uchumi Chuo Kikuu cha Mzumbe, Eliaza Mkuna amesema, Afrika sasa inapaswa kujikita zaidi katika kuboresha mitaala ya elimu ambayo imejikita kwenye masuala ya umahiri uelewa na vitendo ili kuendana na kasi ya ongezeko la rasilimali watu. “Bado tunahitaji nguvu kubwa kuwekeza na kuendeleza mitaala ambayo inajikita hasa kwenye masuala ya umahiri,” na kuongeza kuwa “umahiri nikimaanisha kwamba elimu ambayo itachochea zaidi ujuzi, uelewa na vitendo katika kile ambacho watu wanakisomea.”
Naye rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo, amesema uwekezaji katika raslimali watu ndio moyo kwa mataifa ya Afrika hususani vijana, hivyo mkutano wao umelenga katika kutambua ni aina gani ya uwekezaji unahitajika ili kuleta tija na kuchochea maendeleo ya bara la Afrika.
“Tumekutana leo kujadili ajenda ambayo ndio moyo wa mataifa yetu uwekezaji katika raslimali watu hususani vijana mkutano wetu huu wa leo utaamua ni aina ipi ya uwekezaji unahitajika ili kuleta tija na kuchochea maendeleo ya bara la Afrika” alisema rais Samia.
Mkutano huo ambao umewakutanisha marais 6 wa nchi za Afrika na makamu wa Rais wanne na viongozi wengine mbalimbali huku Rais Samia Suluhu akisisitiza serikali za Afrika ziwekeze zaidi katika rasilimali watu ili kuepusha vijana kulikimbia bara lao.
Imetayarishwa na Amri Ramadhani, VOA, Dar es Salaam
Forum