Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 04:45

Tanzania na Hungary kushirikiana katika biashara, elimu na utalii


Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiongoza ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo na ujumbe wa Hungary unaongozwa na Rais Katalin Novak.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiongoza ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo na ujumbe wa Hungary unaongozwa na Rais Katalin Novak.

Tanzania na Hungary wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbali mbali ikiwemo, biashara, elimu na utalii na kuimarisha usawa wa jinsia kwa kuwawezesha wanawake.

Haya yalisemwa hivi leo wakati Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipokutana na mgeni wake Rais wa Hungary Katalin Novak ambaye yuko katika ziara ya siku nchini humo.

Katika mkutano wao pamoja na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam marais hao wawili Samia Suluhu Hassan na Katalin Novak walisema wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika nyanja za utalii, usawa wajinsia pamoja na elimu.

Ili kuhakikisha suala la usawa wa jinsia linapewa kipaumbele zaidi katika maendeleo ya mwanamke, Rais Samia Suluhu amesema kuwa wamekubaliana kuunda kamati maalum ambayo itashughulikia suala hilo kwa kina zaidi.

Rais Samia alisema: ‘‘Katika mkutano wetu wa nchi hizi mbili ambao umekuwa na tija kubwa tulipata fursa ya kujadili masuala mbalimbali yenye maslahi kwa pamoja na manufaa ya pande zote kwa nchi zetu mbili na watu.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan (kulia) akiwa na Rais wa Hungary Katalin Novak, Ikulu ya Dar es Salaam, Tanzania. Picha ofisi ya Rais.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan (kulia) akiwa na Rais wa Hungary Katalin Novak, Ikulu ya Dar es Salaam, Tanzania. Picha ofisi ya Rais.

Kwa hakika tumerekebisha dhamira yetu ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zetu mbili katika maeneo ya kimkakati yaliyoainishwa pia tumebadilishana maoni kuhusu jinsi nchi zetu mbili zinavyoweza kuimarisha ushirikiano katika ngazi ya kimataifa.’’

Aidha miongoni mwa maeneo ambayo yametiliwa mkazo wakati wa majadiliano ya marais hao ni eneo la elimu ambapo Tanzania itapata nafasi ya kupeleka jumla ya wanafunzi 30 nchini Hungary na wanafunzi wa tano kutoka Hungary watakuja Tanzania ikiwa ni awamu ya kwanza huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kwa mujibu wa mkataba walio saini marais hao.

Kwa upande wa Rais wa Hungary Katalin Novák amesema elimu ni ufunguo wa maisha katika nchi hizo mbili na ushirikiano huo utawapa nafasi vijana wa hungary na Tanzania kufahamiana na watu pamoja na kujua lugha na hivyo kuwapa fursa ya kufanikiwa zaidi.

Rais Novák alieleza: “Moja ya maeneo makuu ya ushirikiano wetu ni elimu, elimu ni ufunguo wa maisha yetu ya baadae ni hivyo kwa Tanzania na ni hivyo hivyo kwa Hungary na uwezekano wa kutoa vijana wa Hungary na Tanzania siyo tu kujifunza na kusoma katika nchi nyingine lakini pia kufahamiana na watu ili kujua lugha na kwa hilo kuwapa fursa ya kufanikiwa zaidi katika nchi zao.”

Hata hivyo Dkt Eliaza Mkuna ambaye ni msimamizi katika idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Mzumbe amesema ushirikiano huo utakwenda kuinufaisha zaidi Tanzania hasa kwenye suala la Elimu kwa kuzingatia ongezeko la watu na uhitaji wa Elimu ya juu nchini.

Dkt Mkuna ameeleza kuwa:"Nadhani Tanzania itaweza kunufaika zaidi kwa namna ambavyo wigo na ongezeko la watu katika nchi yetu ya Tanzania na uhitaji wa elimu ya juu fursa kama hizi za kielimu zinapotokea zinaendelea kutujenga na kutuimarisha katika kuongeza ujuzi na uelewa wa mambo mbalimbali."

Baada ya mazungumzo ya Rais wa Hungary na mwenyeji wake Rais huyo anatarajiwa kwenda kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Arusha na baadae atarejea nchini kwake kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro Julai 20.

Amri Ramadhani sauti ya Amerika Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG