Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Tanzania wameitaka serikali kutilia mkazo suala la maridhiano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa maslahi ya taifa.
Ushauri huo umetolewa baada ya makamu mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu kukosoa maridhiano ya vyama vya siasa na serikali kwa kusema kuwa bado hayajafikia malengo ya kuleta tija kwa taifa
Ikiwa ni miezi takribani tisa imepita tangu kuanzishwa kwa maridhiano ya kisiasa nchini Tanzania kati ya Serikali ya CCM na vyama vya upinzani kaimu mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Tanzania bara Tundu Lissu ameibuka na kusema kuwa maridhiano hayo bado hayajafikia malengo ya kuleta tija kwa taifa lao.
Tundu Lissu
Akizungumza na sauti ya Amerika Tundu Lissu ameongeza kuwa tangu kuwepo kwa maridhiano hayo bado hakuna mapendekezo yoyote ya kufanya mabadiliko ya kisheria kuhusu mfumo mpya wa uchaguzi utakaokuwa huru pamoja na marekebisho ya katiba hali inayohatarisha kuendelea kuumizwa kwa vyama vya upinzani na wagombea wao.
Lissu amesema: "Hakuna mapendekezo yoyoteb ya kufanya marekebisho ya katiba, kutengeneza mfumo mpya wa uchaguzi utakaokuwa huru na hivyo kuna hatari ya kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao tukiwa na tume hii inayotumia katiba hii na sheria za sasa kuviumiza vyama vya upinzani na wagombea wao kama ambavyo ilitokea 2020.
Mchambuzi wa Mambo ya Kisiasa
Hata hivyo mchambuzi wa mambo ya kisiasa na kijamii kutoka chuo kikuu cha Dodoma Dr. Paul Loisulie ametahadharisha kuwa kama kile kilichokusudiwa hakijatimia kuna hatari ya taifa kuendelea kushuhudia malumbano ya kisiasa na ametoa ushauri kwa Rais Samia kulisimamia jambo hilo ili liweze kufika mwisho.
Loisulie amesema: "Kwahiyo madhara yake ni kwamba kile ambacho kilikusudiwa hakijatimia maana yake ni kwamba tutaendelea kushuhudia malumbano ya kisiasa, malumbano ya kijamii na migawanyiko, Rais aendelee kusimama kidete kwasababu hili ni wazo lake na kwa kweli anapaswa alisimamie lifike mwisho."
Katika siku za karibuni vyama vya upinzani vimepata fursa ya kuonyesha mapungufu katika utawala uliopo madarakani wakati ambao Tundu Lissu anautumia vyema kila anapopata nafasi ya kuzungumza na Watanzania.
Mhadhiri Idara ya Sayansi ya Siasa
Wakati huo huo Deusdedit Osward Mhadhiri msaidizi idara ya sayansi ya siasa kutoka chuo kikuu cha Dodoma amesema kuwa kitendo cha Lissu kutoa kauli hiyo kinaweza kuleta wasiwasi kwa wafuasi wa chama chao kutafuta kauli ya kufuata ambapo ameongeza kuwa maridhiano ni jambo lenye hatua na wala si la mara moja.
Osward amesema: Maridhiano yana hatua hatuwezi kuridhiana na tukayamaliza yote kwa wakati mmoja na ndio maana ukiangalia kwamba yeye haridhii kwahiyo itakuwa ni changamoto kwa wanachama wao wafuate lipi kwahiyo athari kubwa kwa maana ya chama chake kwahiyo maridhiano ndani ya chama yatahitajika.
Ikumbukwe mchakato wa maridhiano ulikuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu na vyama vya upinzani ikiwemo CHADEMA na ACT-Wazalendo, ambavyo viliibeba ajenda hiyo kwa muda mrefu ikisisitiza uwepo wa katiba mpya hata hivyo kitendo cha Tundu Lisu kutoa kauli hiyo ya kubeza maridhiano hayo yanatazamiwa kuvuruga kile kilicho fanyika amemalizia kusema Osward.
Amri Ramadhani sauti ya Amerika Dar es Salaam
Forum