Mkuu wa kituo cha Larissa, ambaye hajatajwa hadharani, alifikishwa mbele ya waendesha mashtaka siku ya Alhamisi wakati upelelezi unaendelea kuchunguza chanzo cha ajali hiyo ambapo treni ya abiria na treni ya mizigo ziliruhusiwa kusafiri njia moja na kugongana uso kwa uso.
Afisa wa polisi alisema Jumatano, mkuu wa kituo alikabiliwa na mashtaka utovu wa nidhamu na uzembe uliosababisha vifo vya watu wengi na majeraha makubwa kutokana na uzembe, shirika la habari la Reuters liliripoti.
Waziri wa uchukuzi Kostas Karamanlis alijiuzulu Jumatano, na kukubali kuwajibika na ajali hiyo.
Wakati alipochukua nafasi hiyo, Karamanlis alisema mfumo wa reli ya Ugiriki "haukuwa katika viwango vya karne ya 21”. "Katika kipindi hiki cha miaka mitatu na nusu tumefanya kila linalowezekana kuboresha hali hii halisi," alisema. “Kwa bahati mbaya, juhudi zetu hazikutosha kuzuia ajali hii mbaya. Hili ni tatizo kubwa sana kwetu sote, hususani mimi ”
Ajari hiyo ya treni ilitokea Jumanne jioni karibu na mji wa Tempe, kiasi cha kilomita 380 kaskazini mwa Athens, mji mkuu wa Ugiriki, katika ajali hiyo watu 43 waliofariki na wengine zaidi ya 80 kujeruhiwa.
Baadhi ya taarifa hii inatoka katika mashirika ya habari ya Associated Press, Agence France-Presse na Reuters.