Watu wanane waliuawa baada ya Pantoni ya kuvusha watu na mtumbwi mmoja kugongana kwenye Ziwa Kivu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), maafisa wa eneo hilo walisema Jumanne.
Wanaume wanne na wanawake wanne waliokuwa kwenye mtumbwi huo walifariki katika ajali hiyo, iliyotokea Jumamosi katika bandari ya Bukavu, waziri wa uchukuzi wa jimbo la Kivu Kusini, Mathieu Alimasi Malumni, aliiambia AFP.
Mtumbwi huo ulikuwa ukielekea Idjwi, kisiwa kilicho katikati ya ziwa kubwa la volcano, ulipogongana na Emmanuel 3, Kivuko kinachosafiri kati ya Bukavu na Goma, mji mkuu wa jimbo jirani la Kivu Kaskazini.
Alimasi alisema miili hiyo ilipatikana Jumanne.
Alisema mtumbwi ulikuwa umejaa kupita kiasi na abiria walikuwa hawajavaa makoti ya kuokoa maisha.