Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 05:10

UN : Afrika bado iko nyuma katika kupunguza vifo vya watoto, kina mama


Mwanamke akiwa amemshikilia mtoto wake mchanga baada ya kuzaliwa na mwengine akiwa ndani ya mashine inayosaidia makuzi ya mtoto aliyezaliwa kabla ya muda wake, Sudan Kusini Aprili 3, 2013.
Mwanamke akiwa amemshikilia mtoto wake mchanga baada ya kuzaliwa na mwengine akiwa ndani ya mashine inayosaidia makuzi ya mtoto aliyezaliwa kabla ya muda wake, Sudan Kusini Aprili 3, 2013.

Takwimu mpya za Umoja wa Mataifa (UN) zinaonyesha kuwa bara la Afrika chini ya jangwa la Sahara liko nyuma likilinganishwa na maeneo mengine duniani katika kupunguza vifo vya watoto na kina mama.

Makadirio ya shirika la afya duniani (WHO) na idara ya Umoja wa Mataifa ya kuhudumia watoto (UNICEF) wamebaini kuwa mizozo, mifumo mibaya ya afya na umaskini ni baadhi ya vigezo ambavyo vinachangia kwa mamilioni ya vifo vya watoto na kina mama vinavyoweza kuzuilika.

Idara hiyo ya UN inasema tangu mwaka 2000, vifo vya watoto vimeshuka kwa takriban mara moja na nusu na kwamba vifo vya kina mama vimeshuka kwa zaidi ya theluthi moja, hali hiyo imetokana na upatikanaji wa huduma nzuri za afya.

Makadirio haya mapya, hata hivyo, yanaonyesha kuwa watoto milioni 6.2 walio na umri wa chini ya miaka 15 walifariki mwaka 2018 na takriban wanawake 300,000 wamefariki kutokana na matatizo yanayohusiana na ujauzito na kujifungua mwaka 2017.

Idara zinaripoti kuwa mwanamke mjamzito au mtoto mchanga anayezaliwa anakufa kila sekunde 11 sehemu fulani duniani, wengi wao kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika.

Peter Salama Mkurugenzi Mtendaji wa Afya ya Umma katika (WHO) anasema wanawake na watoto barani Afrika chini ya jangwa la Sahara wako katika hatari kubwa sana kukumbwa na vifo kuliko katika maeneo mengine yoyote.

“Mwaka 2017, kwa mara ya kwanza, nusu ya vifo vya watoto vilitokea barani Afrika. Kwa sababu ya ongezeko la viwango vya uzazi, tunabashiri kwamba idadi hiyo itafikiia zaidi ya asilimia 60 ya vifo vya watoto vinavyotokea ulimwenguni. Kwa vifo vya kina mama hivi leo, theluthi mbili vinatokea barani Afrika,” anasema Salama.

Salama anasema hatari za maisha kwa mwanamke kufariki kutokana na sababu zinazoambatana na ujauzito ni mmoja kati ya 37 barani Afrika, ukilinganisha na mmoja kati ya 7,800 nchini Australia. Anasema hatari za kujifungua mtoto katika nchi zenye serikali thabiti ni ndogo sana ukilinanisha na nchi ambazo zimeathiriwa na mizozo.

Anasema nchi zenye maendeleo kiasi zinaweza kufanya juhudi kupunguza vifo vya mtoto na kina mama. Anaelezea, mataifa ya Malawi, Zambia, Belarusa, Bangladesh na Cambodia.

“Ni sababu moja ya dhahiri kuwa wamewekeza zaidi katika afya ya uzazi, kina mama, mtoto mchanga na afya ya mtoto. Wanachagua program zinazofaa na wanawekeza kwa mujibu inavyotakiwa. Lakini hii si hadithi yote. Wanawekeza pia katika huduma za msingi za afya na afya kwa ujumla. Kwa kifupi, wanawekeza zaidi katika mifumo ya msingi na yenye kuingiliana,” amesema Salama.

Malengo ya UN ya Maendeleo Endelevu yanalenga kupunguza vifo vya kina mama kwa chini ya 70 katika kila mimba 10000 kwa watoto wanaozaliwa, na vifo vya watoto chini ya miaka mitano vipunguzwe walau 25 kwa kila watoto 1000 ifikapo mwaka 2030.

WHO na UNICEF wanasema dunia lazima ichukue hatua hivi sasa na kuwekeza fedha zaidi zinazohitajik kupunguza vifo hivi.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Khadija Riyami, Washington, DC

XS
SM
MD
LG