Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 19:50

UN yataka pande hasimu Sudan Kusini kufikia makubaliano


Bintou Keita
Bintou Keita

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) kwa masuala ya operesheni za ulinzi wa amani amesema Alhamisi amesikitishwa sana na hali ya kibinadamu nchini Sudan Kusini, na kuzitaka pande hasimu kumaliza mzozo unaoendelea huko hivi sasa.

Bintou Keita ameitaka serikali ya Sudan Kusini na viongozi wa upinzani kwanza kuwaweka mbele raia.

“Wapeni watoto wenu fursa. Kila fursa ya amani, kila fursa ya kuokoa maisha ni vyema itumiwe. Mimi nimesikitishwa sana na ghasia ambazo mzozo huu umezileta dhidi ya wanawake na wasichana nchini Sudan Kusini. Ukatili unaotendwa unavuka viwango na huwezi hata kufikiria,” amesema Keita.

Keita amesema kuzuia ghasia za kijinsia ni haki ya binadamu na suala la afya ya umma.

“Ni vyema tuwe na uwezo wa kuangalia hali hii kuwa ni ya dharura na tuhakikishe kwamba kuna ngazi katika sera ambayo inawajibika pamoja kuzuia,” amesema Keita.

Makoi Phillip Wol, mratibu wa manyanyaso ya ngono yanahusisha jinsia katika ofisi ya rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, amesema utawala wa Kiir una nia ya dhati kutekeleza waraka alitoa saini na Umoja wa Mataifa mwaka 2014.

Wol anasema “rais wa jamhuri amemteua waziri katika ofisi yake kuongoza na kuratibu juhudi za serikali na kufanya kazi na mwakilishi maalum wa katibu mkuu kuhusu manyanyaso ya ngono katika mzozo na Umoja wa Mataifa na mfumo wa UN ni kuhakikisha kuna utekelezaji kamili wa waraka huo unaohusu manyanyaso ya ngono.”

Wol amesema vikosi kadhaa katika jeshi ambavyo viko kote nchini vimepatiwa mafunzo kuzuia manyanyaso ya ngono tangu waraka huo utiwe saini miaka minne iliyopita, lakini ufadhili unahitajika ili kuutekeleza kikamilifu.

Katika mkutano na wana habari, David Shearer, wa tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini amesema kutia saini waraka hakutoshi. Suala la kweli ni jinsi tunatekeleza vipi katika sehemu husika, Shearer amesema.

Shearer amesema UN iko tayari kuipatia serikali ya Sudan Kusini msaada wa kiufundi kuhakikisha kwamba watenda manyanyaso ya ngono wanawajibishwa “kuhakiksiha kwamba wakati watu wanapokamatwa kwa uhalifu wa ngono basi polisi wana uwezo wa kuchukua ushahidi kwa usahihi. Na kwamba mashtaka yanaendeshwa vizuri, mahakama zifanya kazi kwa ufanisi kusudi kuwepo na utaratibu wa haki ambao una maana ya kuondoa kutojali kushtakiwa.”

Mapigano Yanaendelea

Licha ya kutia saini wa mkataba wa kuacha mapigano Desemba mwaka 2017, Keita amesema pande zinazopigana zimekuwa katika mapigano kwenye eneo kubwa la Upper Nile na miko ya Bahr-el-Ghazal katika muda wa wiki chache zilizopita.

Keita ametumia muda wa siku nne akiitembelea nchi hiyo na kukutana na maafisa wa serikali, akiwemo makamu rais wa kwanza Taban Deng Gai.

Afisa wa juu wa Umoja wa Mataifa alikutana na wafanyakazi wa misaada na watu waliokoseshwa makazi ndani ya nchi huko Wau, ambako amesema amepata wasi wasi mkubwa kwa kile ambacho amekiona. Keita amezisihi pande zinazopigana kutafuta amani katika amau ijayo ya mazungumzo ya ngazi ya juu ambayo yatafanyika nchini Ethiopia, na yanatarajiwa mwezi Mei 2018.

“Lakini amani haitapatikana Addis Ababa peke yake. Ni lazima ipatikane katika kila jimbo la nchi ambako kuna ushawishi wa kisiasa kwa ghasia za kijamii ambazo zimekuwa chanzo cha wasi wasi mkubwa na kusababisha vifo vingi katika muda wa miezi kadhaa iliyopita,” amesema Keita.

Shearer amesema wanajeshi waliobaki wa vikosi vya ulinzi wa amani vya kikanda watawasili nchini humo katika wiki zijazo na kuleta nguvu ya ziada kwa kikosi cha kikanda ambacho kilipelekwa Juba.

Sudan Kusini iko katika mwaka tano wa mzozo. Zaidi ya watu milioni mbili wamekoseshwa makazi ndani ya nchi na takriban milioni mbili zaidi wamekimbilia nchi jirani.

XS
SM
MD
LG