Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Novemba 21, 2024 Local time: 09:21

Ufisadi uliokithiri Ghana unachukua 20% ya bajeti ya serikali - TI


Rais wa Gana Nana Akufo-Ado
Rais wa Gana Nana Akufo-Ado

Kulingana na ripoti ya shirika la Transparency International  ya mwaka  2023, mataifa mengi ya Afrika yanashuhudia kudumaa kwa juhudi za kupambana na ulaji rushwa, au kushindwa kupiga hatua dhidi ya ufisadi.

Ufisadi bado upo katika nchi nyingi za Afrika, ikiwemo Ghana. Kulingana na Tume ya Haki za Kibinadamu na Haki ya Utawala nchini (CHRAJ) ufisadi unachukua takriban asilimia 20 ya bajeti ya taifa. Mashirika ya kiraia yanajiunga katika vita hivyo, kwa nia ya kufichua vitendo vya ulaji rushwa, na kushinikiza watu wote kuchukua hatua.

Wanahabari hawa wa Ghana wanaonekana wakijiandaa kwa ajili ya ripoti yao kubwa ijayo ya uchunguzi. Wanafanya kazi kwa The Fourth Estate, shirika lisilo la faida la Accra, mradi wa maslahi ya umma na uwajibikaji na taasisi ya Vyombo vya Habari kwa Afrika Magharibi. Kofi Enchill ni mhariri wa The Forth Estate.

“Tunafanya kazi na Waghana; tunafanya kazi na watoa taarifa ambao wanatupa taarifa na hivyo tunaangalia masuala na tunaingia ndani kabisa katika masuala hayo. Tunazitoa kwa kuchapisha, maandishi ya mtandaoni, na video za YouTube na hayo yote, dokumentari za hali ya juu,' anasema.

Wanalenga zaidi hadithi zinazohusiana na kupambana na ufisadi. Tangu kuzinduliwa mnamo 2021 shirika hilo limechapisha hadithi kadhaa za kupinga ufisadi.

Miongoni mwao ilikuwa ni ufichuzi kuhusu mali - kufuatia sharti kwamba maafisa wa serikali watangaze mali zao.

The Fourth Estate iliwasilisha ripoti yake kwa Tume ya Haki za Kibinadamu na Haki ya Utawala ya Ghana ambayo ilichunguza zaidi suala hilo.

"Kwa hivyo, tulipofanya stori hiyo, maafisa wa umma kama 294 walitangaza mali zao haraka. Kwa kweli, kabla ya kuchapishwa, hawakuwa wamefanya hivyo, lakini walikuwa ofisini. Lakini tulipochapisha hadithi hiyo, haraka sana walitangaza mali zao na tulidhani kwamba hiyo ilikuwa na tija, na ilituma ujumbe sahihi kwa mamlaka na maafisa wa umma," anasema Kofi.

Wanaharakati wa kupambana na rushwa wanasema kupambana na rushwa nchini Ghana imekuwa kazi kubwa licha ya nchi hiyo kuzindua Mpango wa Kitaifa wa Kupambana na Ufisadi, waraka wa sera wenye mipango ya kupambana na rushwa.

Mary Awelena Addah, ni Mkurugenzi Mtendaji, Ghana Integrity Initiative. Anasema: “Mpango wa Kitaifa wa Kupambana na Rushwa, ulikuwa ni kielelezo kwetu sote kupambana na rushwa, hata hivyo ungegundua kuwa kuna mapungufu mengi sana ndani ya mfumo huo, ambayo hatukuyazingatia na hiyo inafanya mapambano dhidi ya rushwa kuwa changamoto.”

Kati ya mapungufu hayo ni pamoja na sheria dhaifu zinazokwamisha utendaji kazi wa taasisi za serikali zilizopewa mamlaka ya kuchunguza na kuwafungulia mashitaka viongozi wa serikali wanaofanya ufisadi. Mashirika ya kiraia kama Kituo cha Maendeleo ya Kidemokrasia (CDD) yanajaza pengo hilo. Mnamo 2017, shirika hilo lilizindua Mradi wa Kuangazia Ufisadi katika jaribio la kupunguza ufisadi wa umma kupitia utetezi wa uwazi.

Kojo Pumpuni Asante, Mkurugenzi wa Utetezi na Ushirikiano wa Sera, CDD.

“Tuna uwezo wa kufanya uchunguzi wa awali, tuna waandishi wa habari wachunguzi tukiwa ni sehemu ya timu inayofanya uchunguzi binafsi lakini pia tunajaribu kufuatilia kesi ambazo zipo au kesi ambazo tunahisi zimezikwa na tumesahau kuwa tunahitaji kuzifufua," anasema.

Uanaharakati wa timu ya CCD kwa miaka saba iliyopita unaonekana kuleta tija.

Kojo anasema: "Kwetu sisi, lengo zima kama tulivyosema, hatukutaka suala la ufisadi kufifia, au kuwa la kuzua sokomoko. Tulitaka tu kuweka kwenye akili za wananchi kwamba tunatakiwa kuendelea kupigana, na kuwavutia, wajiunge na mapambano, kwa sababu tulikuwa tunahisi rushwa inazidi kuwa jambo la kawaida, na watu waliona hiyo ndiyo hali ya kawaida.”

Kwa sababu ya kazi za mashirika haya ya kiraia, vita dhidi ya ufisadi viko akilini mwa watu.

"Kama wataalam wa kupambana na rushwa na kutetea utawala bora na taasisi, kazi kubwa imefanywa, tumeonyesha ushahidi wa utafiti kwamba rushwa ni suala nyeti na gumu, na ili kupambana nalo tunahitaji kujitolea kwa dhati," amnasema Mary.

Kulingana na Transparency International, vita vya Ghana dhidi ya ufisadi vimedumaa kwa miaka minne iliyopita. Katika orodha yake ya Ufisadi ya mwaka jana, (CPI), Ghana ilipata sufuri kwa mwaka wa nne mfululizo, bila kupata mafanikio yoyote katika kupambana na rushwa. Nchi hiyo ilishika nafasi ya 70 kati ya nchi na maeneo 180 yaliyochunguzwa kwa kipindi hicho. Kwa wachambuzi wengi, kuwawajibisha maafisa wa serikali wafisadi kupitia mfumo wa sheria itakuwa hatua muhimu katika vita dhidi ya ufisadi.

-Ripoti imeandaliwa na Isaac Kaledzi anaripoti kutoka Accra, Ghana

Forum

XS
SM
MD
LG