Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 05:31

Uchaguzi Mkuu 2022: Mahakama ya Juu Kenya yaanza kusikiliza kesi nane zinazopinga ushindi wa Ruto


Mwenyekiti wa IEBC Wafuta Chebukati akimkabidhi William Ruto hati ya ushindi wa urais baada ya kutangaza matokeo.
Mwenyekiti wa IEBC Wafuta Chebukati akimkabidhi William Ruto hati ya ushindi wa urais baada ya kutangaza matokeo.

Mahakama ya Juu nchini Kenya siku ya Jumatano imeanza kusikiliza kesi nane zilizounganishwa za kupinga matokeo yaliyomtangaza William Ruto mshindi wa uchaguzi wa urais.

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga ambaye ndiye mlalamikaji mkuu katika kesi hii ameweka wazi shutuma dhidi ya tume ya uchaguzi IEBC kwa kusimamia mchakato uliosababisha kupunguzwa kwa kura zake na idadi sawa ya kura hizo kuongezwa katika kura za William Ruto, ambaye ametangazwa kuwa Rais mteule na IEBC.

Mahakama hiyo ya majaji 7 imesikia kuwa mfumo wa teknolojia ya uchaguzi wa IEBC uliingiliwa na raia wa kigeni wakiwemo raia wa Venezuela na watu wengine akiwemo msaidizi binafsi wa Wafula Chebukati ambaye aliingia katika mfumo huo ingawa hakutangazwa kwenye gazeti rasmi la serikali.

Katika uwasilishaji uliofanyika Jumatano mbele ya Jaji Mkuu Martha Koome na majaji Philomena Mwilu, Dkt Smokin Wanjala, William Ouko, Isaac Lenaola, Mohammed Ibrahim, na Njoki Ndungu, mawakili wa Bw Odinga na Martha Karua ambao ni James Orengo, Julie Soweto, Philip Murgor, Pheroze Nowrojee na Paul Mwangi, wameieleza mahakama kuwa uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 9 hauafiki viwango vya kisheria kwa mujibu wa Kifungu cha 138 (3) (c) na 138 (10) cha katiba ya Kenya.

Bw Orengo, katika tathmini yake iwapo Rais Mteule aliyetangazwa alipata kura 50%+1 ya kura zote zilizopigwa, ameeleza kuwa hesabu hiyo ilitokana na hesabu isiyo sahihi ya jumla ya kura zilizopigwa kama ilivyotangazwa na IEBC kwani kuna jumla ya zaidi ya kura 140,000 ambazo hazijulikani zilipo na kwamba kulikuwa na udanganyifu wa hali ya juu.

Bw Orengo, anadai kuwa katika uchaguzi huu palikuwa na hila na njama na mpango wa makusudi kudukua mfumo wa kiteknolojia wa tume ya uchaguzi na kuwekwa matokeo bandia.

Na kuhusu iwapo kulikuwa na tofauti zisizoelezeka kati ya kura zilizopigwa kwa wagombea urais na nafasi nyingine za uchaguzi, iwapo kulikuwa na tofauti kati ya Fomu 34A zilizowekwa kwenye Tovuti ya Umma ya IEBC. Na jingine kuwa Fomu 34A zilizopokelewa katika Kituo cha Kitaifa cha Kujumlisha Kura ya urais katika ukumbi wa Bomas na kuhusu iwapo kulikuwa na tofauti kati ya Fomu 34A zilizotolewa kwa mawakala wa vyama katika Vituo vya Kupigia Kura, Julie Soweto ameieleza mahakama kuwa takwimu zilizopo kwenye fomu zimefanyiwa ujanja na ni tofauti kabisa licha ya kuwa na nembo, mihuri na saini za mawakala wa vyama.

Aidha, ameeleza kuwa katika vituo vyote 41 vya kupigia kura vilivyochukuliwa kama sampuli na kuambatanishwa na hati ya kiapo, kura za Bw Odinga zilipunguzwa na kupewa Bw Ruto, lakini idadi ya wapiga kura ilisalia ilivyo, hasa katika majimbo ya Bomet, Kiambu, Kakamega, Nairobi na Baringo.

Mgombea urais na makamu wake wa Azimio la Umoja, One Kenya, Raila Odinga na Martha Karua.
Mgombea urais na makamu wake wa Azimio la Umoja, One Kenya, Raila Odinga na Martha Karua.

Mfano, Soweto anadai, kuwa Nakala za fomu 41 za 34A ambazo zinaonyesha hitilafu kubwa za kura kutoka Bomet, Kiambu na Kakamega zilizopewa mawakala zinatofautiana na zile za IEBC na zilizowasilishwa katika Kituo cha Kitaifa cha Kujumlisha kura, Bomas jijini Nairobi. Ameeleza mahakama kuwa zaidi ya kura 33,000 zimepunguziwa Bw Odinga na kuongezewa Ruto.

Na iwapo teknolojia iliyotumiwa na IEBC ilikidhi viwango vya uadilifu, uthibitisho, usalama na uwazi ili kuhakikisha matokeo sahihi na yanayoweza kuthibitishwa, na iwapo kulikuwa na ujanja wa upakiaji na usambazaji wa Fomu 34A kutoka vituo vya kupigia kura hadi seva ya IEBC, Philip Murgor amewaeleza majaji hao kuwa mfumo wa teknolojia ya uchaguzi wa IEBC uliingiliwa na raia wa kigeni wakiwemo raia wa Venezuela na watu wengine akiwemo msaidizi wa kibinafsi wa Wafula Chebukati aitwaye Dickson Kwanusu ambaye aliingia katika mfumo huo ingawa hakutangazwa kwenye gazeti rasmi la serikali, na kuhakiki fomu 1, 743 za 34A zilizo na matokeo ya kura kutoka vituo vya kupigia kura.

Bw Murgor pia, ameeleza kuwa kuna ushahidi kwamba fomu zilizokuwa zinawekwa kutoka vituo vya upigaji kuwa, zilikuwa zinazuiliwa zinapakuliwa na kuwekwa upya na maelezo mapya baada ya kubadilishwa katika muundo unaoweza kuhaririwa. Kwa mfano, Abdi Dahir, ambaye hajatangazwa kwenye gazeti rasmi la serikali, pia anadaiwa kuhakiki fomu 659 za 34A.

Aidha, Murgor anaeleza kuwa kulikuwa na ufikiaji wa mbali kwa mfumo wa IEBC siku 3 baada ya shughuli ya kupiga kura kukamilika, huku Okiya Omtatah akisema katika ushahidi wake kuwa hali hiyo ilisababisha kutupwa kwa kura zipatazo 508,647 ambazo zilimwezesha Ruto kufikia alama ya asilimia 50%+1.

Ripoti ya amri kwa tume ya uchaguzi kuwezesha ufikiaji wa seva yake, nakala za sera yake ya usalama ya mfumo wa teknolojia inayojumuisha nenosiri na maingilio kwenye seva hiyo, watumizi wa nenosiri la usimamizi wa mfumo huo, watumiaji wa mfumo na viwango vya ufikiaji, na mawasiliano yaliofanyika kwenye seva hiyo pamoja na nakala halali za Fomu 34A na 34B Kitabu cha 2 zilizotumiwa katika uchaguzi pamoja na kufunguliwa kwa masanduku ya kura katika vituo 15 ili kukaguliwa, kuchunguzwa na kuhesabiwa upya katika majimbo ya Kericho, Mombasa, Nandi na Nyandarua ili kuthibitisha madai kuwa kura ziliibiwa, itawasilishwa mahakamani Alhamisi.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Nairobi, Kenya.

XS
SM
MD
LG