Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 23:46

Mahakama ya Juu Kenya yaamuru kura za Urais kuhesabiwa upya katika vituo 15


Maafisa wa uchaguzi na mawakala wa vyama wakithibitisha kujumlisha kura katika kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura cha tume ya uchaguzi jijini Nairobi, Kenya Jumamosi, Agosti 13, 2022.(AP).
Maafisa wa uchaguzi na mawakala wa vyama wakithibitisha kujumlisha kura katika kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura cha tume ya uchaguzi jijini Nairobi, Kenya Jumamosi, Agosti 13, 2022.(AP).

Mahakama ya Juu nchini Kenya imeamuru kuhesabiwa upya kwa kura za urais katika vituo 15 kote nchini humo, zoezi ambalo limepangwa kuanza mchana wa siku ya Jumanne, Agosti 30, 2022 na litachukua saa 48 kuhakiki kura hizo.

Mahakama ya Juu nchini Kenya imeamuru kuhesabiwa upya kwa kura za urais katika vituo 15 kote nchini humo, zoezi ambalo limepangwa kuanza mchana wa siku ya Jumanne, Agosti 30, 2022 na litachukua saa 48 kuhakiki kura hizo.

Mahakama hiyo katika kikao cha awali cha kesi ya kupinga matokeo ya kura ya urais yaliyomtangaza William Ruto kuwa mshindi, imeamuru tume ya uchaguzi nchini humo IEBC kuwezesha ufikiaji wa seva yake, nakala za sera yake ya usalama ya mfumo wa teknolojia inayojumuisha nenosiri na maingilio kwenye seva hiyo, watumizi wa nenosiri la usimamizi wa mfumo huo, watumiaji wa mfumo na viwango vya ufikiaji, na mawasiliano yaliofanyika kwenye seva hiyo pamoja na nakala halali za Fomu 34A na 34B Kitabu cha 2 zilizotumiwa katika uchaguzi.

Majaji hao pia wameiagiza IEBC kutoa fursa ya kufunguliwa kwa masanduku ya kura katika vituo 15 ili kukaguliwa, kuchunguzwa na kuhesabiwa upya katika majimbo ya Kericho, Mombasa, Nandi na Nyandarua ili kuthibitisha madai kuwa kura ziliibiwa.

Katika kikao hicho cha awali cha kesi ya kupinga matokeo ya kura ya urais ya Agosti 9, yaliyomtangaza William Ruto kuwa mshindi wa kura hiyo, majaji hao saba wa mahakama hiyo ya juu nchini Kenya wakiongozwa na Jaji Mkuu Martha Karambu Koome, wameamuru tume ya uchaguzi kuwezesha ufikiaji wa seva yake ya mfumo wa kiteknolojia, nakala za sera yake ya usalama ya mfumo huo inayojumuisha nenosiri au nywila na maingilio kwenye seva hiyo, watumizi wa nywila za usimamizi wa mfumo huo, watumiaji wake na viwango vya ufikiaji vilivyokuwapo, na mawasiliano yaliofanyika kwenye seva hiyo pamoja na nakala halali za Fomu 34A zilizotumiwa katika uchaguzi huo wa urais.

Mahakama vile vile inaitaka IEBC iwezeshe ufikiaji wa seva zote zilizokuwa katika Kituo cha Kitaifa cha Kujumlisha matokeo ya kura ya urais katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi zilizohifadhi na kusambaza taarifa za upigaji kura na ambazo ni picha za kitaalamu za kunasa nakala ya Fomu 34C ambayo ni hifadhi ya jumla ya kura zilizopigwa.

Wafula Chebukati na tume, wanatakiwa kutoa fursa ya kufunguliwa kwa masanduku ya kura katika vituo 15 vya upigaji kura ili kufanyiwa tathmini, kuchunguzwa na kuhesabiwa upya katika majimbo ya Kericho, Mombasa, Nandi na Nyandarua ili kuthibitisha madai kuwa kura zilifanyiwa ulaghai. Zoezi linalohitajika kufanyika na kukamilika katika kipindi cha saa 48 baada ya maagizo hayo kutolewa, Jumanne hii.

Isitoshe, IEBC inatakiwa kuwasilisha fomu zote zilizotiwa saini na Bw Chebukati zinazoonyesha iwapo palikuwa na hitilafu wakati wa zoezi la kujumlisha na kuthibitisha matokeo ya kura ya urais katika Kituo cha Kitaifa cha Kujumlisha Matokeo hayo ukumbi wa Bomas jijini Nairobi, kati ya tarehe 10 hadi Agosti 15, 2022 wakati ilipomtangaza Ruto kuwa mshindi wa kura hiyo.

Vile vile, tume hiyo inatakiwa kuwasilisha nakala zilizothibitishwa za majaribio ya kutathmini uingiaji wa Mfumo wa Teknolojia ya uchaguzi kabla na wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Urais ikijumuisha nakala zilizoidhinishwa za ripoti zote zilizotayarishwa kwa mujibu wa Kanuni za uchaguzi za mwaka 2017 kwa mujibu wa katiba ya Kenya.

Mwishowe, IEBC inatakiwa kuwasilisha mikataba ya ushirikiano na washirika wake wa kiufundi, orodha ya watumiaji, njia, na ufikiaji wa msimamizi ili kutoa ufafanuzi kuhusu mifumo ya IEBC na matumizi yake kwa ukaguzi na uthibitishaji, kutathmini usalama wa mfumo huo.

Je, maagizo hayo yaliotolewa yanawanufaishaje walalamikaji. Alex Manyasi, mfuatiliaji wa mfumo wa uchaguzi nchini Kenya, anasema “Inaweza kuwa na effect kwa ile kesi ambayo iko katika mahakama,” anasema Manyasi.

Mahakama hiyo imeorodhesha masuala saba yatakayopigiwa darubini katika usikilizaji wa kesi hii inayopinga ushindi wa Bw. Ruto, kutathmini iwapo Rais Mteule aliyetangazwa alipata kura 50%+1 ya kura zote zilizopigwa, iwapo teknolojia iliyotumiwa na IEBC ilikidhi viwango vya uadilifu, uthibitisho, usalama na uwazi ili kuhakikisha matokeo sahihi na yanayoweza kuthibitishwa, iwapo kulikuwa na ujanja wa upakiaji na usambazaji wa Fomu 34A kutoka vituo vya kupigia kura hadi seva ya IEBC, iwapo kulikuwa na tofauti zisizoelezeka kati ya kura zilizopigwa kwa wagombea urais na nafasi nyingine za uchaguzi, iwapo kulikuwa na tofauti kati ya Fomu 34A zilizopakiwa kwenye Tovuti ya Umma ya IEBC na Fomu 34A zilizopokelewa katika Kituo cha Kitaifa cha Kujumlisha Kura, na Fomu 34A zilizotolewa kwa Mawakala katika Vituo vya Kupigia Kura, iwapo kuahirishwa kwa uchaguzi katika majimbo ya Kakamega, Mombasa na maeneo mengine ya Ubunge kulisababisha kukandamizwa kwa haki za wapiga kura hasa kwa walalamikaji na iwapo kasoro zinazojitokeza ni za kiwango cha juu cha kuathiri matokeo ya mwisho ya Uchaguzi wa Rais na iwapo IEBC ilitekeleza jukumu lake la kuthibitisha, kujumlisha, na kutangaza matokeo kwa mujibu wa Kifungu cha 138 (3) (c) na 138 (10).

XS
SM
MD
LG