Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 10:12

Maoni ya mchambuzi kuhusu mkutano kati ya wabunge wa Marekani na Ruto pamoja na Odinga


Seneta Chris Coons, ambaye aliongoza ujumbe wa wabunge na maseneta wa Marekani, akizungumza na Associated Press, baada ya kuitembelea zahanati ya Tabitha Medical Clinic katika kitongoji cha Kibera mjini Nairobi, Agosti 18, 2022.
Seneta Chris Coons, ambaye aliongoza ujumbe wa wabunge na maseneta wa Marekani, akizungumza na Associated Press, baada ya kuitembelea zahanati ya Tabitha Medical Clinic katika kitongoji cha Kibera mjini Nairobi, Agosti 18, 2022.

Wabunge na maseneta wa Marekani wamekutana Alhamisi na rais mteule wa Kenya na mpinzani wake mkuu Raila Odinga, kwa sababu Marekani haitaki Kenya itumbukiye tena kwenye machafuko ili kulinda maslahi yake katika taifa hilo la Afrika mashariki, mchambuzi wa siasa za Kenya na Marekani amesema.

Seneta Coons ambaye alikuwa anaongoza ujumbe huo wa wabunge na maseneta alikutana na vigogo hao wawili waliowania urais, wakati mmoja wao Raila Odinga alipinga matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9, yaliyotangazwa mapema wiki hii na tume ya uchaguzi na mipaka (IEBC).

Mapema jana Alhamisi, Coons alikutana na rais Uhuru Kenyatta ambapo walifanya majadiliano.

Profesa David Monda ambae ameongea na Sauti ya Amerika akiwa mjini Mombasa, anasema mkutano huo una shabaa ya kidiplomasia na kisiasa upande wa Marekani.

“Marekani inataka kuonyesha kwamba iko karibu na Kenya kwa wakati huu ambapo kuna hali ya kutatanisha baada ya Odinga kuwasilisha kesi mahakamani ya kupinga matokeo ya uchaguzi,” amesema David Monda.

“Kisiasa, Seneta Coons wa Jimbo la Delaware yuko karibu sana na Rais Joe Biden, kwa hivyo Marekani ina maslahi mengi ya kulinda nchini Kenya,” ameongeza.

“Kwa nini Marekani haijampongeza rasmi Ruto?”

Kwa mujibu wa Profesa David Monda, Marekani inajizuia kumpongeza rais mteule William Ruto ili kuepusha dosari iliyotekea miaka ya nyuma ambapo baadhi ya maafisa wa zamani wa serikali ya Marekani waliharakia kuidhinisha matokeo ya uchaguzi wa mwaka wa 2017 wakati kulikuwa kesi mahakamani ya kuchunguza uhalali wa matokeo hayo.

“Nadhani Marekani inachukua tahadhari ili isikosee tena kama Seneta John Kerry, waziri wa zamani wa mambo ya nje, ambaye aliharakia kuidhinisha matokeo ya uchaguzi wa 2017 ambao baadaye ulibatilishwa na mahakama ya juu ya Kenya,” amesema Profesa Monda.

Monda anasema haamini kuwa vurugu zitatokea licha ya kwamba Odinga alipinga matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9.

Anasema uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa wa wazi ikilinganishwa na uchaguzi wa miaka iliyopita, licha ya dosari iliyotokea wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi, ambapo maafisa wanne wa IEBC walipinga kuidhinisha matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati.

Ripoti hii imeandaliwa na Patrick Nduwimana.

XS
SM
MD
LG